Ronaldo: United hawakustahili kutufunga

Mtanzania - - Mbele -

BAADA ya Manchester United kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Juventus kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo, amedai hawakuwa na sababu ya kupoteza mchezo huo.

Ronaldo amedai walikuwa na kila sababu ya kushinda mchezo huo kuanzia mabao matatu hadi manne, lakini walishindwa kutumia nafasi hizo na hatimaye wakajikuta wanapoteza baada ya wapinzani wao kutengeneza nafasi mbili na kuzitumia.

Juventus walikuwa wakwanza kupata bao katika dakika ya 65 lililofungwa na Ronaldo, lakini huku zikiwa zimebakia dakika tano mchezo huo kumalizika, Juan Mata aliwainua mashabiki kwa kupachika bao la kusawazisha kutokana na mpira wa adhabu, huku dakika ya 89 nyota wa Juventus, Alex Sandro akijifunga na kumpa jeuri ya kuongea kocha wa Man United, Jose Mourinho.

Hata hivyo, mbali na Juventus kupoteza mchezo huo, lakini wamefanikiwa kufuzu hatua ya makundi, huku wakiwa vinara katika kundi lao H, wakiwa na pointi tisa, wakifuatiwa na Man United wenye pointi saba.

“Nina furaha kuona natoka uwanjani huku nikiwa nimefunga bao, lakini tumejisikia vibaya kupoteza mchezo huo kwa sababu tulikuwa na nafasi ya kufunga mabao matatu hadi manne,” alisema Ronaldo.

Hata hivyo, mchezaji huyo aliweka wazi kuwa, Manchester United, ambaye ni timu yake ya zamani, haikuwa kwenye ubora, lakini walikuwa na bahati na kufanikiwa kushinda mchezo huo.

“Kwa maoni yangu Man United hawakuwa bora, kwa kuwa walitengeneza nafasi mbili, nazijua timu za nchini England, wamekuwa wakitumia nafasi nyingi kwa mipira iliyokufa, lakini tumejifunza kutokana na makosa na tunafurahi kwa kuwa tunaongoza kundi, hivyo tunaweza kusema sisi ni bora,” aliongeza.

Ronaldo alikuwa mchezaji wa Manchester United tangu 2003 hadi 2009, alifanikiwa kucheza jumla ya michezo 196 ya Ligi Kuu England na kufunga mabao 84, kabla ya kujiunga na Real Madrid hadi wakati wa kiangazi mwaka huu alipojiunga na Juventus.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.