Mahakama yaagiza Mbowe, Matiko wakamatwe

Mtanzania - - Habari / Tangazo - Na KULWA MZEE

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kuwakamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ili wafike mahakamani kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana.

Pia mahakama hiyo imeamuru kesi inayowakabili washtakiwa hao na wenzao saba kuendelea kusikilizwa bila kuwakilishwa na Wakili Peter Kibatala.

Mahakama iliamuru pia kuendelea kwa usikilizwaji wa kesi hiyo bila kuwepo kwa washtakiwa wawili, Mbowe na Matiko.

Uamuzi huo wa Mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ulizua utata mkubwa hadi washtakiwa kugoma kujibu lolote na Wakili wa mshtakiwa, Mchungaji Peter Msigwa, Jamhuri Johnson kuamua kujitoa kwa sababu ya kutoridhishwa na mwenendo wa kesi hiyo. Awali akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai washtakiwa Mbowe na Matiko hawapo, wameendelea kuruka dhamana, hivyo aliomba hati ya kuwakamata itolewe na upande wa mashtaka uruhusiwe kuendelea kusoma maelezo ya awali bila wao kuwepo. Wakili John Mallya aliyemwakilisha Wakili Kibatala ambaye alidai anaumwa, alipinga kusomwa kwa maelezo ya awali akidai wadhamini wametoa sababu ya kutokuwepo mahakamani kwa washtakiwa.

Alidai Mbowe yuko Dubaï kwa matibabu na Matiko yuko Burundi kwa ziara ya kibunge, hivyo aliomba kesi isiendelee kusikilizwa.

Hakimu Mashauri alipotoa uamuzi alikubaliana na hoja za upande wa mashtaka hivyo aliruhusu kesi iendelee na mahakama ilitoa hati ya kumkamata Mbowe na Matiko.

Wakili Nchimbi alianza kuwakumbusha washtakiwa mashtaka 13 yanayowakabili kwa kuwasomea upya ambapo kwa nyakati tofauti majibu yalikuwa kama ifuatavyo:

Msigwa: Alikana kuhusika

kuwashawishi wakazi wa Kinondoni kuandamana Februari 16 wakiwa na silaha, lakini aligoma kujibu maelezo ya awali kwa sababu mwakilishi wake Johnson hakuwepo.

“Kabla ya kukumbushwa mashtaka niliomba kushauriana na wakili wangu ukanikatalia... Sasa unajiongoza wewe, nimemtafuta wakili kwa gharama kubwa, lakini na yeye kajitoa, nahitaji kuwa na mwakilishi ndio nitajibu,” alidai Msigwa.

Salum Mwalimu: Mheshimiwa Hakimu sijaelewa kinachoendelea, nipewe muda wa kumtafuta mtu wa kuniongoza, huyu Mallya simwelewi.

John Mnyika: Siwezi kujibu lolote mpaka nishauriane na wakili wangu, naomba uandike hivyo na kwamba maelezo sikuyasikiliza.

Dk. Vicent Mashinji: Nina mwakilishi, nahitaji kuwakilishwa na wakili wangu.

Halima Mdee: Siwezi kujibu chochote mpaka wakili wangu awepo. Esther Bulaya: Naomba nipewe muda wa kuwasiliana na wakili wangu, nimetoka Dodoma mheshimiwa, nafika hapa nasikia wakili Kibatala anaumwa.

John Heche: Siwezi kujibu lolote bila wakili wangu.

Baada ya majibu hayo Hakimu Mashauri alisema mshtakiwa wa pili alikana mashtaka, lakini washtakiwa wengine wote waliokuwepo mahakamani walitaka wakili wao awepo ndio wajibu.

WAKILI AJITOA

Baada ya kukumbushwa mashtaka Wakili wa Msigwa, Johnson aliomba muda wa kushauriana na mteja wake, lakini hakupata nafasi hiyo.

Wakili Johnson alidai anaomba kujitoa kumwakilisha mteja wake akidai kwamba ana miaka 20 ndani ya kazi ya uwakili hajawahi kuona mwenendo wa kesi ukiendeshwa kama kesi hiyo. Alijitoa na mahakama ilikubali, akatoka nje.

Johnson ni wakili wa pili kujitoa kumwakilisha Msigwa. Wa kwanza alikuwa Jeremiah Mtobesya ambaye alijitoa Agosti 23, mwaka huu baada ya kudai kwamba akiendelea kumwakilisha haki haitatendeka.

Washtakiwa wote waligoma kusaini maelezo yaliyoandikwa na hakimu baada ya kumaliza kusomwa maelezo ya awali wakidai hawawezi kufanya hivyo bila mawakili wao.

Wakili Mallya anayemwakilisha Kibatala pia alikataa kusaini akidai matakwa ya sheria ya uwakili yanamkataza kufanya hivyo kwani alimshikia na hakutakiwa kuendelea na mwenendo wowote.

Mahakama baada ya kutoa uamuzi wa kusikiliza kesi, kuamuru Mbowe na Matiko wakamatwe iliahirisha kesi hadi Novemba 12 kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ambao wote ni viongozi wa Chadema, wanaotetewa na Wakili Kibatala ni Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar) na Mnyika (Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba), Heche (Mbunge wa Tarime Vijijini), Mdee (Mbunge wa Kawe), Bulaya (Mbunge wa Bunda), Matiko (Mbunge wa Tarime Mjini) na Dk. Mashinji (Katibu Mkuu).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.