Madiwani Ilala wailalamikia Tarura

Mtanzania - - Habari - Na NORA DAMIAN

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wameulalamikia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura), kwa madai kuwa inachagua barabara za kutengenezwa.

Wakala huo ambao uliundwa mwaka jana una jukumu la kusimamia barabara za vijijini na mijini, ambazo awali zilikuwa zikisimamiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Wakizungumza jana wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani walisema mipango kazi ya wakala huo haieleweki na kusababisha wakose majibu ya kero kwa wapigakura wao.

Diwani wa Kata ya Segerea, Edwin Mwakatobe (Chadema) alisema utaratibu wa matengenezo ya barabara haueleweki na kwamba hawashirikishwi kutoa mapendekezo yao.

“Tuna malalamiko mengi dhidi ya Tarura, mambo hayafanyiki na fedha zinaenda. Barabara ikikatika ukimpigia mkurugenzi anakuambia uwasiliane na Tarura, lakini ukiwasiliana nao wanasema hawana bajeti,” alisema Mwakatobe.

Diwani wa Kata ya Upanga Magharibi, Adinari Kondo (CCM), alisema tangu wakala huo uanze kufanya kazi hawajui vigezo vinavyotumika kuainisha barabara zinazohitaji matengenezo.

“Kwenye kata yangu mwaka 2015/2016 halmashauri ilipanga kuweka lami Barabara ya Mtaa wa Mindu, lakini tangu Tarura walipoingia hakuna kilichofanyika,” alisema Kondo.

Diwani wa Kata ya Majohe, Waziri Mwenevyale (Chadema), alisema katika kata yake barabara inayoanzia Moshi Bar hadi Kwa Mkolemba ilitakiwa iishe Julai mwaka jana, lakini kila anapofuatilia Tarura anaambiwa hakuna fedha iliyotengwa.

Kutokana na hali hiyo Meya wa Manipaa ya Ilala, Charles Kuyeko (Chadema), aliahidi kuunda kamati kukutana na Waziri wa Tamisemi na Mkurugenzi Mkuu wa Tarura kupata majibu ya kero husika.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Jumanne Shauri, alisema wameanza kuwaalika Tarura katika vikao vyao ili kujibu kero zinazohusu miundombinu ya barabara.

Awali Meneja wa Tarura Wilaya ya Ilala, Injinia Samwel Ndoven, alisema wana uhitaji mkubwa wa fedha, lakini bajeti inayotengwa bado ni ndogo.

Kulingana na meneja huyo, katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 Tarura inatarajia kutumia Sh bilioni 6.2 kwa matengenezo ya kawaida na miradi maalumu na kwamba baadhi ya miradi taarifa zake za manunuzi zimekamilika.

“Tunashirikiana sana hasa wakati wa kuandaa bajeti, lakini uhitaji ni mkubwa na uwezo bado ni mdogo. Tunapenda barabara zote zitengenezwe kwa lami, lakini tutajitahidi kwa kidogo kinachopatikana,” alisema Injinia Ndoven.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.