Zinahitajika hatua madhubuti soko la korosho

Mtanzania - - Tahariri -

KWA wiki kadhaa sasa kumekuwapo na sintofahamu kuhusu ununuzi wa korosho za wakulima nchini. Hiyo ni kutokana na wafanyabiashara kusita kama si kugoma kununua korosho hizo kwa bei elekezi ya Sh 3,100 kwa kilo.

Kwa sababu hiyo, ni jambo la faraja kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusema Serikali inaendelea na mazungumzo na mataifa mbalimbali yaweze kununua korosho nchini.

Tatizo la ununuzi wa korosho mwaka huu lilianza baada ya wafanyabiashara kutaka kununua zao hilo kwa bei ya chini ya Sh 2,000 kwa kilo, hatua iliyowafanya wakulima kukataa kuuza.

Hali hiyo ilisababisha Rais John Magufuli kuingilia kati na baada ya kuwa na kikao na wadau mbalimbali wa zao hilo, aliweka bei ya zao hilo kuwa Sh 3,100 kwa kilo moja.

Wakati ilitegemewa kuwa huenda uamuzi huo ungesaidia kuendeleza ununuzi wa zao hilo, badala yake wafanyabiashara wakaamua kususa.

Hadi sasa minada ya zao hilo inapoitishwa katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya kusini, wafanyabiashara wamekuwa wakigoma kununua korosho kwa bei hiyo elekezi ya Sh 3,100.

Ni hali ambayo haikutarajiwa na ambayo inazidi kuwaweka wakulima katika wasiwasi mkubwa kuhusu hatma ya korosho zao kwa msimu huu.

Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba korosho kuendelea kukaa katika maghala ubora wake unapungua polepole.

Lakini kubwa zaidi ni kwamba matarajio yao ya kupata fedha kugharamia mahitaji yao mbalimbali nayo yanazidi kufifia na kuzidi kuwaweka katika wakati mgumu.

Vilevile huwa inategemea kuwa wakulima wanapouza korosho zao mapema huwapa fursa ya kuona mwelekeo na jinsi ya kujiandaa kwa msimu ujao.

Kwa maana hiyo, kadiri siku zinavyokwenda ndivyo wanazidi kukabiliwa na wasiwasi mkubwa kuhusu maisha yao kwa ujumla kwa sababu ya kutojua nini cha kufanya.

Ndiyo sababu tunasema tamko la Waziri Mkuu Majaliwa bungeni Dodoma jana kuwa Serikali iko kwenye mazungumzo na mataifa mbalimbali yaweze kununua zao hilo ni hatua nzuri.

Ni muhimu basi suala hilo liharakishwe wananchi hao waweze kupata afueni ya kuuza korosho zao na hivyo kutekeleza masuala mbalimbali ya familia zao na maisha yao kwa ujumla.

Pamoja na hayo, pengine ingefaaa suala zima la kilimo cha korosho liangaliwe upya kuanzia maandalizi ya mashamba, ununuzi wa dawa na upulizaji wake, uvunaji, uhifadhi na uuzaji.

Tunasema hivyo kwa kutambua kwamba miongoni mwa mambo ambayo yalisababisha tatizo la ununuzi wa korosho na bei kuwa ndogo – kabla ya Rais Magufuli kuingilia kati – ni mvutano uliokuwapo kuhusu bei ya dawa za kupulizia korosho. Kwa upande fulani, hali hiyo ilisababisha wakulima wachelewe kuinunua dawa hiyo na pengine hata kupunguza ubora wa zao hilo.

Kwa korosho, dawa ya kuulia wadudu ni muhimu katika kuchangia ubora wa zao hilo, hivyo suala hilo halina budi kuangaliwa kwa kina na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kabla ya kuanza msimu ujao wa kilimo.

Lakini pia mfumo wa kuuza korosho nao hauna budi kuangaliwa upya na kuona jinsi gani unavyoweza kuimarishwa kwa manufaa ya wakulima na taifa zima kwa ujumla, ikizingatiwa hivi sasa mataifa mengi zaidi duniani yanalima korosho ambayo inaelezwa huuzwa ikiwa katika kiwango cha juu cha ubora.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.