Hospitali ya Benjamin Mkapa inavyopiga hatua

Mtanzania - - Mtazamo -

WAKATI Tanzania ikitimiza miaka mitatu ya mabadiliko ya kiutendaji na mafanikio chini ya Serikali wa Awamu ya Tano, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa, mwaka huu imefanya mageuzi katika kutoa huduma za afya baada ya kufanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa wanne, hii ikiwa ni mara ya kwanza tangu hospitali hiyo ianzishwe.

Upandikizwaji huo wa figo umefanywa na Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Tokushukai Medical Corporation na Tokyo Women’s Medical University kutoka Japan.

Huduma ya upandikizaji figo katika hospitali hiyo zilianza Machi mwaka huu, ambapo mgonjwa mmoja alipandikizwa figo na baadaye mwezi Agosti wagonjwa wengine watatu walipandikizwa figo, huku mgonjwa wa tano akitarajiwa kupandikizwa figo Desemba mwaka huu.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Egid Beatus Mubofu, anasema kuwa UDOM kwa kushirikiana na washirika wa mpango wa huduma za upandikizaji figo imejizatiti kutoa mafunzo kwa wataalamu wa magonjwa ya figo ili kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa mafanikio makubwa zaidi hospitalini hapo.

Profesa Mubofu anasema kuimarika kwa huduma za afya za kibingwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, kunaleta mapinduzi makubwa katika huduma za afya katika Mkoa wa Dodoma, ambao kwa sasa una wakazi wengi baada ya Serikali kuhamia huko.

“Niwahakikishie watumishi wanaohamia Dodoma kuwa wasiwe na wasiwasi kuhusu huduma za afya, kwa kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo pia ni Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma imejipanga kuwapatia huduma za afya za uhakika,” anaeleza Prof. Mubofu.

Mafanikio ya hospitali hiyo yanatokana na uhusiano uliopo kati ya UDOM na Shirika la Tokushukai Medical Corporation la nchini Japan, baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kusaini makubaliano ya ushirikiano mwaka 2003.

Kupitia uhusiano uliopo kati ya Mkuu wa Chuo, Rais Mstafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Hospitali za Tokushukai Medical Corporation yenye Hospitali zaidi ya 75 nchini Japan na sehemu nyingine duniani, Dk. Tokuda Tarao, Chuo Kikuu cha Dodoma kilipatiwa msaada wa mashine 10 za kusafishia damu (Haemodialysis) mwaka 2010.

Wakati huduma ya kusafisha damu (Haemodialysis) inaendelea kutolewa na Hospitali ya UDOM kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa mafanikio makubwa, mwaka 2016, Uongozi wa UDOM kupitia Wizara ya Afya uliiomba Tokushukai Medical Corporation kusaidia katika kuanzisha huduma ya upandikizaji figo katika Mkoa wa Dodoma. Ombi hilo lilikubaliwa na maandalizi ya mwanzo yalianza kwa kuwapeleka watalaamu wa Kitanzania nchini Japan kwa mafunzo ya miezi mitatu kuanzia Mei hadi Julai, 2017.

Ushirikiano wa UDOM na Tokushukai katika zoezi hili ni wa miaka minne kuanzia 2017 hadi 2021, ambapo wataalamu kutoka Japan watakuwa wanakuja nchini kusaidia kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na wataalam wa Tanzania kwenda Japan kwa ajili ya kujengewa uwezo zaidi.

Profesa Mubofu anaeleza kupatikana kwa huduma za upandikizaji figo hapa Dodoma kumeiwezesha Serikali kuokoa fedha ambazo zingetumika kwa gharama za kupeleka wagonjwa wa figo nje ya nchi.

Anasema kumpeleka mgonjwa mmoja nchini India kupata huduma ya kupandikiza figo inagharimu kiasi cha Sh milioni 77 mpaka milioni 80, lakini mgonjwa mmoja kufanyiwa upandikizaji wa figo hapa nchini inagharimu Sh milioni 22, hivyo kuokoa fedha nyingi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk. Aliphonce Chandika, anasema kuwa huduma hiyo ya upandikizaji figo itakuwa endelevu. Ametoa wito kwa Watanzania kufika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu na uchunguzi.

Aidha, Dk. Chandika ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kununua vifaa vya kutosha kwa ajili ya Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambapo kwa kiasi kikubwa vifaa hivyo vinasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi na kuokoa fedha nyingi za Serikali.

Dk. Chandika anakishukuru Chuo Kikuu cha Dodoma na Madaktari bingwa kutoka Tokushukai Medical Corporation na Tokyo Women’s Medical University kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa katika kufanikisha upasuaji na upandikizaji huo wa figo.

Hospitali ya Benjamin Mkapa inakuwa hospitali ya pili kutoa huduma ya upandikizaji wa figo. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndiyo hospitali ya kwanza kuanza kutoa huduma za kupandikiza figo hapa nchini.

Niwahakikishie watumishi wanaohamia Dodoma kuwa wasiwe na wasiwasi kuhusu huduma za afya, kwa kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ambayo pia ni Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma imejipanga kuwapatia huduma za afya za uhakika

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.