Wenzi waishi kwa kula matunda, waacha kuswaki

Mtanzania - - Furahi Dei - HASSAN DAUDI Na MITANDAO

WATAALAMU wa afya duniani kote wanasisitiza juu ya umuhimu wa matunda, wakisema binadamu anapaswa kula matunda kila siku bila kupata ushauri wa daktari.

Lakini je, umewahi kujiuliza itakuwaje ikiwa mtu ataamua kuyafanya matunda kuwa ndiyo mlo pekee?

Kwamba, kuanzia asubuhi hadi usiku anapokwenda kulala awe anakula mapapai, maembe, machungwa au matunda mengine na si chai, ugali au wali kama ilivyozoeleka.

Tina Stoklosa (39), na mpenzi wake, Simon Beun (26), wameamua kuishi hivyo, wakidai matunda yana umuhimu mkubwa kuliko chakula chochote.

Walianzaje, waliwezaje na ni faida zipi walizozipata kwa uamuzi wao huo wa kuishi kwa kutegemea matunda? Soma makala hii iliyotafsiriwa kutoka gazeti la Daily Mail la Uingereza.

Wakazi hao wa Bali nchini Italia, wanasema wana miaka mitatu sasa tangu walipouanza utaratibu huo uliowashangaza wengi katika mitandao ya kijamii.

Tina ambaye ni mzaliwa wa Warsaw, Poland, anasema mbali ya kumfanya awe mwenye nguvu na mwonekano wa ujana, pia kula matunda kumemsaidia kupunguza uzito, tatizo lililomsumbua kwa miaka mingi alipokuwa akiishi nchini Uingereza.

“Nilikuwa na tatizo la uzito kwa kipindi chote cha umri huu wa utu uzima. Nilipambana kwa kweli, nikijaribu kula vyakula vyenye mpangilio maalumu lakini sikufanikiwa. Kila mwaka nilijiona naongezeka tu, sikuona msaada wowote.

“Kipindi hicho nilikuwa na uzito wa kilo 82 lakini utaratibu wa kuishi kwa kula matunda umenisaidia, nimepungua na sasa nina kilo 50,” anasema Tina.

Anasema licha ya kuwa na umri wa miaka 36 kipindi hicho, hakuwa na mpenzi, jambo ambalo anahisi lilitokana na ‘ubonge’ wake kutowavutia wanaume.

“Wakati nikihangaika kutafuta suluhisho, nikakutana na msichana mmoja katika mitandao, ambaye alisema amekuwa akiishi kwa kula matunda tu. Hapo pia nililikuta kundi kubwa la watu wanaofanya hivyo, wakijiita ‘walaji matunda’.

“Wengi wao walionekana ni wenye afya na walikuwa na nguvu, na wapo waliokuwa wanamichezo. Nilivutiwa nao na kuanzia hapo nikaamua kuwafuata ili kujaribu kupunguza uzito kwa kula matunda,” anasema.

Ukiacha hilo la uzito, Tina anasema ulaji wa matunda umewasaidia kuepuka tatizo la msongo wa mawazo, ambalo limekuwa likiwasumbua wengi.

“Ulaji wa matunda huondoa msongo wa mawazo, hutibu magonjwa mengine ya akili, pia husaidia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula,” anadai.

Cha kushangaza zaidi, si tu kuacha vyakula vyote na kubaki na matunda, pia wapenzi hao hawanywi maji, juisi wala soda, na badala yake wamekuwa wakitumia maji ya nazi kukata kiu.

Kilichowaacha hoi wengi mitandaoni ni kwamba wameacha hata utaratibu wa kupiga mswaki, wakidai kuwa ulaji wa matunda mara kwa mara una msaada mkubwa katika kusafisha meno yao.

Kwa upande wa mwenza wake, Simon, ambaye ni raia wa Ubelgiji, anasema haikuwa rahisi kuzoea utaratibu huo wa kuacha vyakula vingine na kuishi kwa kutegemea matunda, lakini alijiapiza kuwa hatarudi nyuma katika maisha mapya aliyoyaanza.

“Sikutaka kurudi nyuma, kula vyakula vya kawaida. Haikuwa rahisi lakini kwa miaka miwili ya mwanzo niliona kabisa kuwa nimefanikiwa kutokula chakula kilichopikwa,” anasema.

Aidha, katika wale waliofuatilia mtindo huo wa maisha ya Tina na Simon, wapo waliotumia akaunti zao za mitandao ya kijamii kudai kuwa ulaji wa matunda umewasaidia kupona ugonjwa hatari wa saratani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.