Marita Lorenz alivyomtafuta mwanawe - 7

Mtanzania - - Kisima Cha Ujuzi - Na MARKUS MPANGALA

SIKU chache baada ya kurejea Marekani, Marita Lorenz, alipokea wageni wanne kutoka shirika la upelelezi wa ndani la FBI, walitembelea nyumbani kwa dada yake Valerie.

Wanausalama wa FBI walimhoji kwa saa kadhaa na Marita Lorenz aliwaeleza kila kitu juu ya Fidel Castro na mwanawe Andres Castro.

Alichowaeleza FBI wale walikuwa wanaandika, ambapo zilifika kurasa 18. Baada ya kumaliza kuandika vijana wa FBI walimwambia Marita Lorenz kwamba wanafahamu alichosema ni ukweli mtupu, kwa sababu nao walikuwapo ndani ya jengo lile. Hilo lilimshangaza Marita hivyo alirudisha kumbukumbu na kugundua kuwa nyumba ile inafuatiliwa na CIA.

Baada ya hapo Marita Lorenz alifunga safari kwenda New York kumwona mtoto wake mwingine Monica ili amshawishi warudi Florida na kumsimulia habari za Andres.

Wakiwa katika mgahawa mmoja ghafla alihisi hali tofauti mara baada ya kumaliza kunywa kahawa. Monica alimsaidia kutembea, akaita taksi na kwenda hospitali ambako walihisi aliwekewa sumu aina ya Scopolamine.

Marita anasema wasiwasi ulimkumba zaidi pale mtu asiyejulikana alipolipia gharama za kahawa. Pia mtu asiyejulikana alilipia gharama zake za matibabu hospitalini.

Mtu huyo alihakikisha hakuna rekodi za Marita Lorenz kulazwa hospitalini. Akahisi serikali ilikuwa nyuma ya matukio hayo – yote yalimtatiza.

Kitu kimoja ambacho Marita hakufahamu baada ya kuonana na Andres ni kwamba mama yake alificha barua yenye picha ya mwanawe akiwa mdogo.

Marita aligundua picha hiyo mara baada ya kifo cha mama yake ambapo ilifichwa sandukuni.

Barua yenye picha ilitumwa kwake katika kipindi ambacho Marita alikuwa kwenye operesheni mbalimbali.

Mwaka 1990 Marita wakati akiendelea na mikakati ya kutengeneza filamu ya historia yake alikutana na matajiri wawili Sarah na Laura huko Hollywood.

Awali alishatibuana na watu wawili; Anna Meizer wa Ujerumani na Oliver Stone. Wawili hawa walitaka kutengeneza dokumentari ya maisha yake kabla ya mpango kuvunjika.

Sarah na Laura walipanga mikakati ya filamu ya historia ya Marita. Marita akapewa mwaliko wa kuhudhuria kongamano la mazingira nchini Nicaragua. Marita alitakiwa kuhudhuria kongamano hilo kwa niaba ya Sarah na Laura.

Marita akaamua kumpigia simu mwanawe mwingine Monica aliyekuwa akiishi California ili waende wote Nicaragua.

Siku chache kabla ya Marita kwenda Nicaragua alipewa taarifa kuwa mwaliko huo umefutwa bila kujua sababu za kufutwa kwake, dili likafa.

Hata hivyo, Marita akaendelea na mpango wa kwenda Nicaragua. Akiwa nchini humo alitembelea Hospitali ya Karl Marx mjini Managua. Huko alifuatilia taarifa za daktari Andres raia wa Cuba.

Wauguzi na madaktari wa hospitali hiyo walimmwagia sifa kemkemu za daktari Andres, bila kujua Marita ndiye mama yake.

Mwishowe Marita akabaini kuwa jina kamili la mwanawe ni Andres Vazquez Castro. Ni mtoto wa Marita na Fidel Castro. Alifanya kazi nchini Nicaragua kwa nyakati tofauti.

Mwaka 1998 mwandishi wa habari Wilfried Huismann kutoka jiji la Bremen nchini Ujerumani alimpigia simu Marita kwa lengo la kutoa wazo la kutengeneza filamu.

Kipindi alichojitokeza Willy, hali ya Marita haikuwa nzuri, alikuwa anajiuguza baada ya kufanyiwa upasuaji.

Mpango wa filamu ulimlazimu Marita kusafiri kwenda nchini Cuba kwa mara nyingine. Lengo ni kukusanya taarifa mbalimbali ziwe sehemu filamu hiyo.

Machi 5, 2000 Marita na Willy waliwasili jijini Havana (Cuba). Wakiwa Cuba walitakiwa kusubiri kibali cha kurekodi filamu kutoka serikalini, lakini kubwa zaidi ni kufanya mahojiano na mkuu wa usalama Fabian Escalante na Fidel Castro.

Hata hivyo, wote wawili walikataa ombi hilo bila kueleza sababu. Willy akakata tamaa, kwani hakutegemea kukataliwa.

Marita alitamani kukutana tena na Andres Vazquez, lakini hakuwa na mawasiliano naye.

Filamu ilipangwa kuitwa ‘Dear Fidel’, lakini kipande cha Fidel Castro kisingekuwapo baada ya kukataa mahojiano.

Willy na Marita wakasonga mbele, sasa wakiwa wamepanga kumtafuta na kumhoji Diaz Yanez Pelletier, mtu mtiifu na mwaminifu kwa Fidel Castro.

Marita aliamini akikutana na Yanez utakuwa mwanya wa kumshawishi Fidel Castro kukutana tena.

Marita anakumbuka urafiki wa Yanez na Castro ulivunjika mwaka 1960 na alitupwa jela miaka 15. Baadaye alitolewa na utawala wa Castro. Sasa alimhitaji ili watengeneze filamu hiyo.

Mazungumzo baina ya Marita na Yanez yalichukua saa chache licha ya Castro kufanya juhudi za kuzuia filamu hiyo.

Yanez hakujua kama kuonana na Marita kisha kukubali kuhojiwa ni kosa. Septemba mwaka 2000 Yanez alifariki, ambapo Marita anaamini aliuawa.

Katika simulizi hii, Marita Lorenz ana mtoto mwingine anayeitwa Monica ambaye alizaa na Rais Marcos Perez Jimenez wa Venezuela kabla ya kutekelezwa msituni na baadaye kuokolewa na CIA.

Sarah na Laura walipanga mikakati ya filamu ya historia ya Marita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.