Elimu haki za abiria kutolewa kuanzia shuleni

Mtanzania - - Kisima Cha Ujuzi - Na CHRISTINA GAULUHANGA

ELIMU ya usalama barabarani imekuwa ikitolewa kwa muda mrefu kuanzia ngazi ya familia nchini kote ili kupunguza vifo na ajali zinazosababishwa na uzembe wa madereva.

Zipo sababu na vikwazo kadhaa vinavyochangia abiria kudhurumiwa haki yao pindi wanapokuwa safarini.

Hali hiyo imekuwa ikichangiwa na uoga au ukosefu wa uelewa wa abiria kujitambua na kufahamu haki zao na wajibu pindi wanapokuwa safarini.

Utafiti wa Baraza la Usimamizi Watumiaji Huduma za Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC), ulionyesha asilimia 54 ya watumiaji wa usafiri wa barabara na reli hawajui haki na wajibu wawapo kwenye usafiri.

Tatizo hilo linatoa fursa kwa wadau wengi ndani na nje ya nchi kuwekeza katika eneo hilo muhimu la kutoa elimu kwa jamii ili kuokoa maisha ya wananchi wengi ambao wamekuwa wakipata ulemavu, kupoteza maisha na hivyo familia nyingi kubaki yatima.

Pia wapo ambao wamejikuta kila kukicha wakinyanyasika kwa kupitishwa vituo au kutozwa nauli mara mbili kwa ruti moja kwa sababu ya uoga au kukosa elimu sahihi ya usalama barabarani.

Ukosefu wa elimu hiyo ambao unazalisha uoga, hofu kutothubutu kutoa taarifa au kukemea mwendokasi unapelekea ongezeko la ajali za barabarani.

Ofisa Elimu wa usalama barabarani kutoka SUMATRA CCC, Nicholous Kinyariri, anasema hata watumiaji wale wanaojua haki na wajibu wao bado wanakosa uthubutu na ujasiri wa kuongea juu ya maslahi yao mbele ya kondakta na dereva wa daladala.

Mfano, nauli zimeandikwa ubavuni kwenye mlango wa kuingilia ndani ya daladala na kwenye tiketi anayopewa abiria. Pia, daladala zimeandikwa mbele kituo cha kuanzia na kuishia na zina rangi za njia zinakopita. Hayo yote ni matangazo rasmi ya mamlaka kuonyesha nauli harali na vituo halali vya kuanzia na kuishia. Lakini bado utaona abiria wanazidishiwa nauli na daladala kukatisha ruti wanakaa kimya bila kukemea au kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tamwa), Gladnes Munuo, anasema zipo sababu nyingi zinazoleta vichocheo kwa abiria kunyanyaswa ndani ya usafiri.

Anasema Tamwa imekuwa ikitoa elimu kwa wadau ili waweze kufahamu haki zao pindi wanapokuwa barabarani.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (Taboa) Mustapha Mwalongo,

anasema kupenda urahisi kumekuwa kukichangia vitendo vya unyanyasaji kwa abiria.

Anasema sheria za Sumatra zinaelekeza wazi haki za abiria na watoa huduma ya usafiri.

Anasema cha ajabu abiria wamekuwa wakiwaruhusu makondakta na madereva kufanya mambo yaliyozuiliwa na mamlaka kwa sababu ya wao kutaka urahisi.

Anatoa mfano wa suala la ukatishaji tiketi, abiria ameelekezwa aende kwenye ofisi ya mabasi lakini wapiga debe wamekuwa wakitumia fursa hiyo kuuza tiketi njiani na kusababisha wengi wao kudhurumiwa hasa katika kipindi

cha mwisho wa mwaka.

Dereva Idrisa Musa, anayeendesha daladala lifanyalo safari Gongo la Mboto Simu2000 anasema yapo baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakisababisha abiria na watoa huduma kuendelea kuumia kila kukicha.

Anasema kitendo cha kondakta kutoa fedha na kumpa mpiga debe ni mfumo ambao umekuwa ukiwaumiza lakini yote hiyo ni kwa sababu ya mamlaka zinazohusika kushindwa kuwaondoa wapiga debe vituoni.

“Mamlaka zinazohusika wakisimama vyema katika vituo vya mabasi na kuwaondoa wapiga debe nafikiri kero hii sugu itaondoka kwani sisi tunalazimika kuwapa fedha kwani wakati mwingine wanatuishia hata visu,” anasema Mussa.

Anasema kuhusu abiria kutozwa fedha mara mbili inatokana na ujanja wa kuongeza mapato angalau wafikie hesabu ya tajiri.

“Bila kutoza fedha ya mzunguko mara mbili madereva wote wangekuwa wamerejesha magari kwa mabosi kwani fedha yote inakata barabarani na ukizingatia faini haziishi kosa dogo tu la kuonywa unashangaa unapigwa makosa hata mawili,” anasema Mussa.

Abiria Jacquelin Harold mkazi wa Kinyerezi anasema, hakuna unyanyasaji wanaofanyiwa na madereva hasa katika nyakati za asubuhi na jioni.

Anasema kipindi hicho madereva na makondakta ndio kwao wanakiita kama cha kuchuma au kujipatia fedha nyingi kwakuwa wamekuwa wakitoza fedha mara mbili wakiamiani abiria wanawahi kwenda kazini na kurejea nyumbani.

Kinyariri anasema baraza hilo limeamua kuondoa tatizo hilo kwa kutoa elimu kwa wanafunzi shuleni, wenyeviti wa serikali za mitaa, makundi yenye uhitaji maalum, wakulima na wafugaji kwa kutumia vyombo vya habari machapisho, mikutano ya wazi mikoani na nyimbo mbalimbali.

Abiria wakisubiri usafiri katika moja ya vituo nchini

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.