TPDC wajenga vyoo vya wanafunzi Kilwa

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limejenga vyoo bora katika

Shule ya Msingi Kivinje, iliyoko Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyoo hivyo, Meneja Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu, alisema shirika lao linatambua umuhimu wa kuisaidia jamii ili kuisaidia Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali.

“Sisi kama shirika la umma, tunao wajibu wa kurudisha sehemu ya kile tunachopata kwa jamii zetu hizi ili kuweza kuboresha maeneo mbalimbali ya huduma hasa ya afya, elimu, maji na utawala bora.

“Kwa hiyo huo ujenzi wa vyoo bora kwa wanafunzi wa shule hii ya Kivinje unaangukia katika maeneo yote mawili ya elimu na afya.

“Suala la vyoo bora kwa wanafunzi ni muhimu hasa katika kuwapa faraja na kujiamini zaidi wawapo shuleni na hivyo kusababisha umakini zaidi katika masomo yao,” alisema Msellemu.

Akielezea maendeleo ya ujenzi wa vyoo hivyo, Msellemu, aliwahimiza watendaji wa shule hiyo pamoja na kamati ya ujenzi, kuongeza kasi ya ujenzi ili vikamilike mapema.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa, Ramadhani Hatibu, alisema ameridhishwa na jinsi ambavyo TPDC wanavyoshirikiana nao katika kusaidia uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.