EPZA yapokea wawekezaji kutoka Misri

Mtanzania - - Biashara - Na GUSTAPHU HAULE

MAMLAKA ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), imewapokea wawekezaji wakubwa zaidi ya 25 kutoka nchi ya Misri ambao wamekuja nchini kwa ajili ya kuangalia fursa ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali.

Timu ya wawekezaji hao imewasili jana katika mamlaka hiyo ikiwa chini ya kiongozi wa msafara ambaye pia ni mwenyekiti wa Shirikisho la Wawekezaji wa Viwanda nchini humo, Dk. Sherif El Gabaly na kufanya mkutano wa pamoja na viongozi wa EPZA.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwezeshaji Wawekezaji kutoka EPZA, James Maziku, aliwaambia wawekezaji hao kuwa, Tanzania bado ina fursa kubwa ya uwekezaji na inawakaribisha katika kuwekeza katika viwanda mbalimbali.

Alisema Serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda, ndiyo maana imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kwa kuhakikisha sehemu ya uwekezaji kunajengwa miundombinu mizuri ya maji, umeme, barabara na mahitaji mengine muhimu.

Aliwaeleza wawekezaji hao kwamba, kwa sasa maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika uwekezaji ni Bagamoyo mkoani Pwani, Kigoma, Mtwara na Kurasini Jijini Dar es Salaam na kwamba katika maeneo hayo miundombinu yote ipo sawa na maeneo yapo ya kutosha.

“Tanzania hatuna masharti makubwa kwa wawekezaji, maana tupo katika kuhakikisha tunajenga uchumi wa viwanda, hivyo kwa mwekezaji kutoka nje analazimika kuwa na mtaji unaoanzia dola za Kimarekani 500,000 na mwekezaji wa Kitanzania mtaji wake ni dola 100,000,” alisema Maziku.

Alisema malengo ya mpango wa EPZA ni kukuza pato la fedha za kigeni, kuongeza fursa za ajira, kukuza ushirikiano wa uchumi wa ndani na soko la kimataifa, kuhamasisha teknolojia mpya pamoja na kuhamasisha usindikaji wa malighafi za ndani kwa ajili ya kuzalisha bidhaa za kuuza nje ya nchi.

Kwa upande wake, Dk. Sherif El Gabaly, alisema kuwa, walikuja nchini kwa ajili ya kuangalia fursa ya uwekezaji na kwamba kulingana na maelezo yaliyotolewa na mkurugenzi wa EPZA, yamewafanya kuvutiwa kwa ajili ya kuhakikisha wanakuja kufanya uwekezaji huo kwa haraka.

Alisema makampuni ambayo yapo tayari kuwekeza ni 25, lakini hata hivyo wanakwenda kuhamasisha wengine ikiwa pamoja na kufanya tathmini ili wanapokuja waweze kutekeleza azma yao ya uwekezaji Tanzania.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.