Trump amfukuza mwanasheria mkuu

Mtanzania - - Kimataifa / Matangazo -

SIKU moja tu baada ya kupata pigo katika uchaguzi wa wabunge katikati ya muhula wake, Rais Donald Trump amemfukuza Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, Jeff Session huku akimtimua mwanahabari mmoja kutoka kwenye mkutano wake Ikulu.

Akitoa taarifa kupitia mtandao wa Twitter, Rais Trump alisema nafasi ya Jeff itashikwa kwa muda na Mwanasheria, Matthew Whittaker.

Katika ukurasa wake wa Twitter Rais Trump alimshukuru Sessions kwa kazi yake hiyo na kumtakia kila la kheri.

Kwa upande wake, Sessions katika barua yake ya kujiuzulu, aliweka bayana kuwa uamuzi wa kuondoka kutoka nafasi hiyo haukuwa wake.

Katika barua isiyokuwa na tarehe alimjulisha Rais kwamba anawasilisha barua yake ya kujiuzulu kama alivyomtaka afanye hivyo.

Akimshukuru Trump kwa uamuzi wake huo, alisema cha muhimu wakati wa uongozi wake kama mwanasheria mkuu wa serikali alirudisha na kuimarisha utawala wa sheria.

Kwa mujibu wa Ofisa wa Ikulu ya Marekani, John Kelly, alimuita Sessions Jumanne kabla ya Rais Trump kuitisha mkutano wa habari kujadili matokeo ya uchaguzi wa wabunge uliofanyika juzi.

Mara kwa mara Trump alikuwa akimkosoa Sessions, Seneta wa zamani wa Republican na mfuasi wake wa mwanzo wakati wa harakati zake za kuwania urais.

Dalili za mwanasheria huyo kutimuliwa kazi zilionekana wazi kutokana na Rais Trump kuonyesha uwezekano huo mapema.

Awali, Trump alieleza kutofurahishwa kwake na hatua ya Sessions kujiondoa katika uchunguzi wa FBI kuhusu madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.

Alidai Sessions alikuwa na msimamo dhaifu.

Wakati huo huo, Ikulu ya Marekani imefuta kibali cha uandishi wa Ikulu cha mwandishi wa CNN. Jim Acosta saa chache tu baada ya kujibizana na Rais Trump.

Katika mkutano na wanahabari Ikulu mjini hapa, Mfanyakazi mmoja wa Ikulu alijaribu kunyakua kipaza sauti kutoka kwa mwandishi huyo.

Lakini Mkuu wa Habari wa Ikulu, Sarah Sanders alisema kibali hicho kilifutwa kwa sababu mwandishi huyo alimwekea mwanamke mikono yake.

Hata hivyo, Acosta aliyataja madai ya Sanders kuwa ya uongo.

Rais Trump alimtaja mwandishi huyo kuwa mtu mbaya ajabu wakati wa mkutano huo.

Acosta alimuuliza Trump juu ya hatua za hivi majuzi kuhusu maelfu ya wahamiaji wanaoelekea Marekani kutoka nchi za Amerika ya Kati.

Mfanyakazi mwanamke wa Ikulu alijaribu kuchukua kipaza sauti kutoka kwa mwandishi huyo ili ampe mwandishi mwingine. “Imetosha, imetosha’, Rais alimuambia Acosta, kabla ya kumwambia aketi na kuweka kipaza sauti chini.

Sanders katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa twitter alisema Ikulu haiwezi kuvumilia mwandishi anayemwekea mikono yake mwanamke anayejaribu kufanya kazi yake.

“Kwa sababu hiyo, Ikulu inafuta kibali cha kuingia Ikulu cha mwandishi wa habari aliyehusika kwa muda usiojulikana,” alisema.

CNN ilitoa taarifa kupitia Twitter ikisema amri hiyo ilikuwa ni ya kulipiza kisasi kwa maswali magumu ya Jim Acosta.

“Mkuu wa habari wa Ikulu, Sarah Sander alidanganya, alitoa taarifa za uongo na kutaja kisa ambacho hakikutokea,” ilisema taarifa ya CNN.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.