Sakata la Humud lachukua sura mpya

Mtanzania - - Michezo - Na ZAITUNI KIBWANA

SIKU chache baada ya klabu ya KMC, kutangaza kuachana na kiungo wake, Abdulharim Humud, ameibuka na kusema meneja wake, Antonio Nugaz, anaangalia namna ya kufanya ili aweze kupatiwa haki zake.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba, amefukuzwa KMC kwa madai ya kutaka kuwa katika mahusiano ya kimapenzi na wake, wapenzi wa wachezaji wenzake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Humud, alisema viongozi wa KMC, wameamua kumchafua tu ila wanapaswa kusema ukweli.

Humud aliyewahi pia kuzitumikia klabu za Coastal Union na Azam FC, alisema aliandika barua mwenyewe ya kuomba kuachwa na KMC, baada ya kuona anakosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi kinachonolewa na Etienne Ndayiragije.

“Mimi ni mchezaji ili nionekane kuwa bora, lazima nicheze na siridhiki nichukue mshahara bure bila kuutumikia popote ndio maana niliandika barua mwenyewe ya kuomba niachwe.

“KMC walikubali ila kwa masharti ya kurudisha jezi na vifaa vyote walivyonipa, wakasema watamtafuta mwanasheria wao ili waangalie kama kuna sehemu natakiwa kulipa kwa sababu mimi ndio nimeomba kuvunja mkataba.

“Nashangaa baada ya barua hiyo, wanaibuka na kusema nimechukua wake za wachezaji wenzangu, huku ni kunichafua kwa kuwa hizi ni tuhuma nzito.

“Najiuliza hizi ndizo fadhila zangu za kuipandisha timu? Sipati jibu kwa sababu bao langu la kichwa nililofunga ndilo limeifikisha KMC ilipo sasa, wameamua kunichafua ila nawaambia mimi sitakosa timu ya kucheza kwa uwezo wa Mungu,” alisema Humud.

Upande wake meneja wa mchezaji huyo, Nugaz, alisema tayari wameonana na mwanasheria, Alex Mgongolwa, kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi.

“Nimeshakutana na Mgongolwa ila tunapitia barua zote kwanza, kabla ya kufanya chochote kile kwa sababu kwenye mkataba wa Humud kuna vitu vimekaa vibaya kidogo vya kisheria,” alisema Nugaz.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.