Waandishi waliokamatwa Dar wazua taharuki

Mtanzania - - Mbele - Na ANDREW MSECHU

WAANDISHI wa habari wa kimataifa, Angela Quinter, Raia wa Afrika Kusini na Muthoki Mumo, Raia wa Kenya, waliokuwa wamekamatwa nchini na maofisa wa Idara ya Uhamiaji na baadaye kuachiwa huru, wamezua taharuki ndani na nje ya nchi.

Waandishi hao waliripotiwa kukamatwa juzi usiku na kuachiwa baada ya saa nne usiku, huku hati zao za kusafiria zikiendelea kushikiliwa. Hata hivyo, baadaye walirudishiwa hati zao hizo.

Wawili hao walikamatwa juzi saa 4.00 usiku na waliachiwa jana saa 9.00 alfajiri.

Taarifa ambazo MTANZANIA ilizipata jana jioni kutoka kwa Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, zilieleza kuwa baada ya kurudishiwa hati zao za kusafiria jana jioni, waandishi hao waliamua kuondoka nchini jioni hiyohiyo kwenda Afrika Kusini.

“Mchana wa Novemba 8, 2018 TEF imezungumza na Idara ya Uhamiaji waliosema waandishi hao walikamatwa kwa kuwa walikuwa wakifanya kazi kinyume cha matakwa ya viza inayowaruhusu kuingia nchini.

“Baadaye Balozi wa Afrika Kusini nchini, Thami Mseleku, aliiambia TEF kuwa Angela na Muthoki wameamua kuondoka nchini baada ya kumalizana na idara ya uhamiaji,” alisema Balile katika taarifa yake.

Muda mfupi baada ya kusambaa taarifa za kukamatwa kwao, kituo cha habari cha CNN cha Marekani kilieleza kuwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, ilikuwa inafuatilia kwa karibu taarifa hizo.

“Tunaendelea kuwasiliana na Serikali ya Tanzania katika mambo mengi ikiwamo hili linalohusu haki za binadamu. Marekani inaendelea kuheshimu suala la demokrasia, utawala wa sheria, uhuru wa kujieleza na haki nchini Tanzania,” CNN ilikariri sehemu ya taarifa kutoka Serikali ya Marekani.

Taasisi ya Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ilisema jana kwamba waandishi hao waliokamatwa usiku wa kuamkia jana baada ya kufuatwa na watu wawili hotelini kwao waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa Idara ya Uhamiaji waliachiwa na kukabidhiwa hati zao za kusafiria.

Uhamiaji yatoa ufafanuzi

Jana, Idara ya Uhamiaji ilikiri kuwakamata waandishi hao ambao ni wafanyakazi katika Kamati Maalumu ya Kuwalinda Wanahabari Duniani (CPJ) kwa madai kwamba walikuwa wamekiuka masharti ya hati zao za kuingia nchini.

Katika taarifa yake, Msemaji wa Uhamiaji, Ally Mtanda, alisema wageni hao waliingia nchini Oktoba 31 mwaka huu, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Quintal akitokea Afrika Kusini na Muthoki akitokea Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wawili hao kwa pamoja waliomba na kupatiwa kibali cha matembezi cha miezi mitatu hadi Januari 1, mwaka 2019.

“Baada ya mahojiano, walikiri kwamba wameingia nchini kwa nia ya kufanya vikao na waandishi wa habari wa hapa, wakati vibali vyao ni kwa ajili ya matembezi, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Uhamiaji sura ya 54, rejeo la mwaka 2016 na kanuni za viza za mwaka 2016,” alisema Mtanda.

Taarifa ilieleza jana kuwa baada ya hati zao kushikiliwa kwa muda, jana mchana walikabidhiwa hati hizo kutoka kwa maofisa wa uhamiaji waliowafuata katika hoteli waliyofikia na hawakupewa masharti yoyote kuhusu nyaraka zao za kusafiria na kuhakikishiwa usalama wao wakati wakiendelea na shughuli zao zilizowaleta nchini.

Taarifa nyingine iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri la Afrika (TAEF), ililaani kukamatwa kwa waandishi hao na kushikiliwa kwa zaidi ya saa nne.

Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa TAEF, Jovial Rantao, ilieleza kuwa wanachukulia kitendo hicho kuwa uvamizi wa uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari.

Rantao alisema jana kuwa TAEF imekuwa ikifuatilia kwa karibu ukandamizwaji wa vyombo vya habari unaoendelea Tanzania na kuishukuru Serikali ya Afrika Kusini kwa kuchukua hatua iliyosaidia kuachiwa kwa hati za kusafiria za wanahabari hao.

Rantao alisema pia kwamba TAEF inatambua kazi kubwa iliyofanywa pia na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kufuatilia kukamatwa kwa waandishi hao.

Alisema TAEF inaendelea kutoa wito kwamba Afrika inahitaji vyombo vya habari vilivyo huru, imara na vinavyoweza kutekekeza kwa uhuru majukumu yake kwa kufuatilia taasisi za umma.

Katika taarifa yake, Jukwaa la Wahariri la Kenya lilieleza kushtushwa kwake na taarifa za kukamatwa kwa waandishi hao.

Katika taarifa yao iliyotolewa na kutiwa saini na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Churchil Otieno, ilieleza kuwa wana taarifa kwamba simu na kompyuta mpakato za waandishi hao zilishikiliwa na kuchunguzwa kinyume cha utaratibu.

Chadema wazungumza

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, aliitaka Serikali iwajibike kwa kuheshimu mikataba ya kimataifa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari kwa vitendo.

Alisema ni vema idara ya uhamiaji iwajibike kwa kuueleza umma ni sheria gani iliyotumika kuwakamata waandishi hao ambao waliingia nchini kwa halali na kukutana na viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania.

Mrema alisema ni vema Serikali iboreshe mazingira ya waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhakika na kwa usalama na si kuendeleza vitisho vinavyoendelea kulichafua Taifa.

“Serikali yetu isipokuwa makini katika haya yanayoendelea nchini, itaendelea kuyumba kiuchumi na watalii wataendelea kukimbia na taswira ya nchi itaendeela kuchafuka katika jumuiya ya kimataifa.

“Ni vema Serikali ihakikishe inawashughulikia pia maofisa uhamiaji waliodaiwa kushikilia simu za waandishi hao na kuendelea kuzitumia kwa kutuma ujumbe wa maneno kwenye twitter, hatua iliyoulazimu uongozi wa twitter kufungia akaunti hizo baada ya waandishi hao kulalamika.

Taarifa za kukamatwa kwa wanaharakati hao zilianza kusambaa mitandaoni ndani na nje ya nchi usiku wa kuamkia jana ambako CPJ ilieleza katika akaunti yake ya twitter:

“Tunaitaka mamlaka husika Tanzania, kuwaachia haraka wafanyakazi wetu Angela Quintal na Muthoki Mumo ambao wamechukuliwa na kupelekwa kusikojulikana,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Awali, usiku wa kuamkia jana, katika ukurasa wa twitter wa mwandishi Quintal, ilichapishwa taarifa iliyoeleza kwamba wameachiwa na wamesharudi hotelini ikisema, ‘Mungu ni mkubwa, tumeachiwa tunaenda hotelini.’

Hata hivyo, baadaye taarifa hiyo ilikanushwa kupitia ukurasa wa twitter wa dada yake Quintal aitwaye Genevieve Quintal akisema wanahabari haowalikuwa bado hawajaachiwa kama ilivyoripotiwa awali na anayeandika hayo ni mtu mwingine.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.