Siko tayari kutumbuliwa kwa kutotekeleza wajibu – Waziri Aweso

Mtanzania - - Kanda -

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema hayuko tayari kutumbuliwa kwa kutohakikisha anatekeleza azma ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.

Aweso alitoa kauli hiyo bungeni jana alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kuteuliwa, Salma Kikwete (CCM).

Katika swali lake,Salma alitaka kujua tamko la serikali kuhusiana na utekelezaji wa mradi wa maji wa Lindi ambao umekuwa ukipigwa danadana kuanzia mwaka 2015.

Akijibu, Aweso alisema alipokuwa akiapishwa na Rais John Magufuli alipewa kazi ya kuhakikisha anatatua tatizo la maji kwa kumtua mama ndoo kichwani. Alisisitiza hayuko tayari kutumbuliwa kwa kushindwa kutekeleza jukumu hilo.

“Siwezi kukubali, sipo tayari kutumbuliwa nitahakikisha natekeleza jukumu langu,”alisema.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Latifah Chande (CCM) aliyetaka kujua kauli ya serikali kutokana na ufisadi uliokithiri kwenye miradi ya maji ambayo imekuwa haitoi thamani ya fedha, Aweso alisema:

“Serikali haitamfumbia macho mkandarasi au mtumishi yeyote atakayekula fedha za miradi ya maji na kuwa mtu huyo atazitapika fedha hizo”.

Katika swali la msingi, Chande alisema wananchi wa Mkoa wa Lindi wanakabiliwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu hadi kusababisha baadhi ya wananchi hasa vijijini kutumia maji ya mito na mabwawa pamoja na mifugo.

“Je, ni lini serikali itakamilisha miradi mbalimbali ya maji mkoani Lindi,”aliuliza Chande.

Pia alitaka kujua ni lini serikali itahakikisha upatikanaji wa maji safi katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi kuepusha uwezekano wa magonjwa ya mlipuko kwa wauguzi na wagonjwa.

Akijibu maswali hayo, Aweso alisema katika kukabiliana na uhaba wa maji katika Mkoa wa Lindi, serikali inaendelea kutekeleza miradi maeneo ya mijini na vijijini kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.

Alisema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, miradi ya maji katika vijiji 48 ilikuwa imekamilika huku miradi katika vijiji 21 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Katika kuboresha huduma ya maji mjini Lindi na vijiji vya pembezoni, Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi mkubwa wa maji Ng’apa ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 92 na unatarajia kukamilika Februari mwaka 2019.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.