Boomplay, Universal Music Group kusambaza muziki Afrika

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU

MTANDAO wa kusikiliza (streaming) na kupakua (download) muziki Afrika, Boomplay Music na Universal Music Group (UMG), zimeingia makubaliano ya kushirikiana katika usambazaji wa muziki Afrika.

Akizungumza katika hafla ya utiliwaji saini wa makubaliano hayo, Makamu wa Rais wa UMG, idara ya Maendeleo ya Masoko, Adam Granite, alisema kupitia ushirikiano huo na Boomplay watawawezesha wasanii Afrika kuwa wabunifu katika kazi zao na kuingiza kipato kikubwa zaidi.

Alisema mkataba huo utawasaidia wasanii wa UMG kuwafikia watumiaji wapya, huku wakiongeza hamasa ya usikilizaji wa muziki wa Afrika ili wapate faida kuwafikia mashabiki wa muziki, wasanii wengine na wazalishaji muziki.

“Ushirikiano huu utaendelea kufikia watu wengi na kuhakikisha kazi za wasanii wetu zinawafikia mamilioni ya wapenzi wa muziki barani Afrika,” alisema Granite.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Boomplay, Joe He, alisema Boomplay itaendelea kuunda ushirikiano unaoimarisha mfumo wa kidijitali na kuunganisha wapenzi wa muziki na nyimbo wanazozipenda wakati wowote na mahali popote.

Aliongeza kuwa App ya Boomplay ambayo kwa sasa inapatikana kwa watumiaji wa simu za Android, inatarajia kuzindua app kwenye jukwaa la iOS hivi karibuni ili kuongeza watumiaji wapya.

Boomplay itasambaza muziki kutoka kwa UMG nchini Tanzania pamoja na Nigeria, Ghana, Kenya, Rwanda, Uganda na Zambia. Mpaka sasa, Boomplay ina nyimbo zaidi ya milioni mbili na maelfu ya video zinazopatikana kwa watumiaji wake zaidi ya milioni 36 na watumiaji karibu milioni mbili wanaoongezeka kila mwezi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.