Walio kwenye ndoa walazimishwa mapenzi kinyume cha maumbile

Mtanzania - - Habari - Na OSCAR ASSENGA - TANGA

UKATILI wa kingono na kiuchumi umeelezwa kushamiri mkoani Tanga hususani kwa wanawake walio ndani ya ndoa, ambapo inadaiwa hulazimishwa kufanya mapenzi kinyume cha maumbile.

Hayo yalisemwa juzi na Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake mkoani Tanga (TAWLA), Latifa Ayoub wakati wa semina ya wadau wa masuala ya haki za watoto ambapo walijadili changamoto mbalimbali za ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani humo.

Alisema mbali na wanawake kufanyiwa ukatili huo na wenzi wao ndani ya ndoa watoto wa shule nao hulawitiwa au kubakwa na walimu wakiwamo wa vyuo vikuu, ndugu wa karibu wa familia majumbani.

“Baadhi ya wanawake hupigwa na waume zao au kuachwa hatua ambayo imesababisha watoto wengi kufanyiwa ukatili wa kisaikolojia, kukosa matunzo bora na huwa hawaendi shule hivyo hukosa elimu.

“Tumeona tutoe elimu shirikishi na wadau mbalimbali kuhusiana na masuala ya ukatili wa jinsia shuleni, wazazi na walezi kwa lengo la kubaini vitendo vya hivyo na namna ya kumlinda mtoto kupata haki stahiki”alisema Ayoub.

Awali akizungumza katika semina hiyo, Mratibu wa Dawati la Jinsia wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, Inspekta Yason Mnyanyi alisema kuna aina nyingi za ukatili lakini zaidi kuna ukatili wa kimwili, kisaikolojia ,kingono na kiuchumi.

Alieleza kwamba ukatili wa kingono ni kitendo ambacho anafanyiwa mtu kinacholenga kumuumiza ikiwemo kumshika sehemu za siri bila ridhaa yake, kumbaka au kumlawiti.

Hata hivyo alisema madhara makubwa ya ukatili wa mwili yanaweza kusababisha majereha, kifo ulemavu wa kudumu bila kusahau magonjwa ya zinaa pamoja na ukimwi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.