Bulaya aomba Bunge kuingilia kati mafao

Mtanzania - - Habari / Tangazo - Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), ameliomba Bunge kuingilia kati kanuni za Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa kile alichodai kuwa vikokotoo vya pensheni vinamnyonya mfanyakazi.

Kulingana na Kanuni mpya ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018, hivi sasa watumishi wa Serikali na sekta binafsi watatumia kikokotoo kimoja.

Kabla ya mabadiliko hayo wanachama wa Mfuko wa PSPF na LAPF walikuwa wanalipwa kwa kikokotoo cha 1/540: 15.5 na mkupuo wa asilimia 50 wakati NSSF walikuwa wakipokea asilimia 25 ya michango.

Akizungumza jana, Bulaya alisema mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani yalitaka kikokotoo kiwe 1/480 na lazima kiwepo kwenye sheria.

Hata hivyo aliwalaumu wabunge wa CCM kutumia wingi wao vibaya kupitisha mambo hata kama hayana manufaa.

“Bunge lina mamlaka liweke kipindi cha mpito cha kusimamisha kanuni zisitumike kwanza na kama ikishindikana kama Waziri Kivuli nitapeleka muswada wa kuzibadilisha,” alisema Bulaya.

Alisema kuna malalamiko mengi ya wastaafu kuhusu vikokotoo hivyo huku wengine wakiwa bado hawajalipwa mafao yao.

“Nimekutana na wastaafu zaidi ya 300 wakiwa na malalamiko lukuki, kuna mwingine amestaafu miezi mitatu hajalipwa na michango yake haijarekodiwa.

“Waache kutoa majibu mepesi kwenye hoja nzito, watafute mbadala kwa kufuata taratibu na kuwashirikisha wadau,” alisema.

Alitoa mfano wa nchi nyingine na vikokotoo vyao kwenye mabano kama vile Rwanda (1/480), Uganda (1/500) na Kenya (1/480) kwamba hata kama mtumishi akitaka anaweza akachukua asilimia 100 au 75 kisha asilimia 25 akalipwa kidogo kidogo.

“Ufaransa mifuko inasimamiwa na wafanyakazi wenyewe, yaani nchi za wenzetu wametoa ‘option’ na bado mifuko haifi. Na tulitahadharisha bungeni hawakutaka kusikia,” alisema Bulaya.

Bulaya pia alihoji kwa nini wabunge wakimaliza vipindi vyao wanalipwa fedha zao zote na kukifananisha kitendo hicho kuwa sawa na ubinafsi.

“Kwa nini kile tunachokipata tusiwatetee wengine, na kuna baadhi ya viongozi vijana wanavimba vichwa wanasahau kuna maisha zaidi ya uwaziri…ni wanafiki na wachumia tumbo tu,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.