JET, USAID yanoa wahariri masuala ya hifadhi

Mtanzania - - Habari -

NA MWANDISHI WETU -BAGAMOYO

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wahariri wa habari wa vyombo mbalimbali nchini na kutakiwa kuangalia utunzaji wa bionui kutunza mazingira kwenye hifadhi nchini.

Mafunzo hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki mjini Bagamoyo yakiwa na lengo la kuwanoa viongozi hao wa vyombo vya habari kujua masuala ya uhifadhi, uwindaji na usafirishaji haramu wa wanyamapori unaofanywa na wawindaji haramu.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, alisema mpango wa mafunzo unaratibiwa na JET kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) chini ya mradi wa Protect.

Aliwaomba wahariri kutambua wajibu wa kulinda rasilimali wanyama kama njia ya kukuza utalii nchini.

Alisema hatua hiyo ni awamu ya pili ya mafunzo hayo ambako awamu ya kwanza ilitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kama njia ya kuwajengea uwezo katika kusimamia na kuandika habari za uhifadhi, uwindaji haramu na ukuzaji wa utalii nchini.

Chikomo, alisema chama hicho kimejikita katika kupaza sauti juu ya masuala ya uhifadhi nchini na kuona sekta hiyo inaleta tija katika kukuza uchumi wa nchi.

“Katika hili tunawashukuru wenzetu USAID-Protect kushirikiana nasi kuwajengea uwezo waandishi na wahariri ambao ndiyo wachakataji wakuu wa habari katika vyombo.

“Kama viongozi hao watapata uelewa wa kina kuhusu masuala ya hifadhi sote kwa pamoja tutaweza kuwa kwenye daraja moja la kulinda rasilimali muhimu za nchi ikiwamo wanyamapori,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.