Serikali itafakari kupunguza wafungwa magerezani

Mtanzania - - Habari/ Matangazo - Na JAVIUS KAIJAGE

WAKATI mataifa kadhaa ya Ulaya yakiendelea kufunga magereza yao kutokana na kupungukiwa wafungwa, taifa letu linaendelea kukumbwa na msongamano wa wafungwa/mahabusu magerezani.

Uholanzi ikiwa ni miongoni mwa mataifa ya Bara la Ulaya, mwaka 2016 ilitangaza mikakati ya miaka mitano ijayo kwa kuhakikisha inayafunga magereza yake matano kwa kile kilichotafsiriwa kupungukiwa na idadi ya wafungwa baada ya uhalifu kupungua.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari katika taifa hilo ni kwamba kila mwaka wafungwa wamekuwa wakipungua magerezani kwa asilimia 0.9 kutokana na sababu mbalimbali.

Aliyekuwa Waziri wa Usalama na Sheria wakati huo, Ard van der Steur aliliambia gazeti fulani la nchi hiyo ya kuwa kupungua kwa wafungwa ni matokeo ya wasimamizi wa sheria kutoa adhabu za vifungo vifupi magerezani huku uhalifu wa kutisha ukiendelea kushuka.

Haitakuwa mara ya kwanza kwa Uholanzi kufunga magereza yake kwa sababu ya kupungukiwa na idadi ya wafungwa kwani mwaka 2009 ilifunga magereza manane na mwaka 2015 ikayafunga magereza 19.

Kama Uholanzi imeweza kupunguza wafungwa magerezani naamini wakati umewadia kwa serikali yetu kubuni mikakati kabambe ikiwamo kuiga kutoka kwao ili ipatikane suluhisho la msongamano wa wafungwa/mahabusu magerezani ambao kimsingi ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia haipendezi hata kidogo nchi yetu kuendelea kuwekwa katika kundi la mataifa ambayo watu wake wanaishia magerezani badala ya kuendelea kusherehekea Uhuru.

Wakati Serikali yetu ikiwa na mipango mahsusi ya kuwaletea wananchi maendeleo huku ikihamasisha Jeshi la Magereza kuhakikisha linawafanyisha kazi wafungwa ili waweze kujitegemea basi pawepo na njia nyingine mbadala ya kuwapunguza magerezani ili wakazalishe wenyewe wakiwa huru huko uraiani.

Ni kweli kila taifa lina historia, utamaduni, uchumi, siasa na mazingira yake kwani uendeshaji wa Uholanzi hauwezi kufanana kwa asilimia mia moja na wa Tanzania lakini yapo mambo ya kujifunza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.