Wanafunzi watakiwa kupenda masomo ya sayansi ili kuinua uchumi

Mtanzania - - Habari Za Biashara - Na AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM

SERIKALI imeanza jitihada mbalimbali za kuinua na kuhamasisha watoto kupenda kusoma masomo ya sayansi ili kujenga msingi imara wa kuipeleka nchi katika uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi, wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti na zawadi ya fedha taslimu wanafunzi waliofanya vizuri masomo ya Kemia na Biolojia katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne kwa mwaka 2017 na sita 2018 iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA).

Alisema kutokana na umuhimu wa masomo hayo, serikali imeanza jitihada mbalimbali za kuinua na kuhamasisha watoto kupenda na kusoma masomo ya sayansi, lengo likiwa ni kujenga msingi imara wa uchumi wa kati.

“Kwa kuanza Serikali imeendelea kutoa motisha ya kutoa mikopo ya asilimia 100 kwa wanafunzi wanaochukua michepuo ya sayansi kwenye vyuo vikuu vyetu vyote pamoja na kuendelea kuhamasisha ongezeko la walimu wa sayansi kwenye shule zetu zote nchini,” alisema Profesa Kambi.

Alisema mipango mingine ni pamoja na kuwa na wataalamu waliofundishwa na kufuzu vizuri katika taaluma ya sayansi, hasa Kemia na Baiolojia.

Alisema mwelekeo wa Tanzania ya sasa ni kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025, ambapo serikali inapambana kuweza kuyatimiza maono hayo kwa vitendo.

“Unapozungumzia kuwa na viwanda vya dawa ni lazima uwe na wakemia, wafamasia na mafundi sanifu teknolojia ya maabara kwa ajili ya utendaji kazi katika viwanda hivyo,” alisema Profesa Kambi.

Awali Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, alisema jumla ya wanafunzi 24 na walimu wanne kutoka shule mbalimbali walikabidhiwa zawadi hizo kwa lengo la kuongeza motisha ya ufaulu katika masomo hayo.

Akitaja zawadi hizo, alisema kwa kidato cha sita mshindi kwa kwanza kitaifa kwa masomo hayo atapata Sh 5,00,000, wa pili Sh 450,000, wa tatu Sh 400,000 na vyeti.

Aliongeza kwa upande wa kidato cha nne mshindi wa kwanza amepatiwa Sh 450,000, wa pili Sh 400,000 na wa tatu Sh 350,000.

Alisema watahiniwa waliopata zawadi hizo kwa kufanya vizuri zaidi kitaifa katika somo la Kemia kidato cha nne kwa mwaka 2017 kwa wasichana wametoka katika Shule ya Wasichana ya Marian (Pwani), wa pili ametoka Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis (Mbeya) na wa tatu ametoka Shule ya Wasichana ya Sayansi Kandoto (Kilimanjaro).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.