TPA kupakua tani milioni 25 za mizigo kwa mwaka

Mtanzania - - Habari Za Biashara - Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

UPANUZI wa Bandari ya Dar es Salaam (TPA) utaiwezesha kuhudumia shehena za mizigo tani milioni 25 kwa mwaka kutoka tani milioni 16 za sasa.

Mradi huo unaohusisha ujenzi wa gati namba moja hadi saba sambamba na kuongeza kina cha bahari ulianza Juni mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Juni 2020.

Akizungumza juzi, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Fred Liundi, alisema kabla ya upanuzi wa bandari hiyo ilikuwa na uwezo wa kupokea tani milioni 13.5, lakini mwaka jana ziliongezeka na kufikia tani milioni 16.2.

“Hitaji la kupanua bandari yetu lilikuwa la msingi kuwezesha kuipa uwezo wa kuhudumia wateja wa ndani na nje, hivyo tunatarajia baada ya kumaliza upanuzi itakuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni 25 za mizigo,” alisema Liundi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, alisema upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam unalenga kuifanya kuwa ya kisasa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, hivi sasa uwezo wa bandari hiyo ni kupokea magari 2,500, lakini baada ya maboresho hayo wataweza kupokea magari 10,000 kwa wakati mmoja.

“Hii ina maana magari ambayo tumewahi kuyapokea miaka ya nyuma tangu kuanza kwa TPA yatapita zaidi ya mara mbili. Kwa mwaka tunaweza kupokea magari zaidi ya 259,000 ukilinganisha na magari 190,000 tuliyowahi kuyapokea 2013/2014,” alisema Kakoko.

Kuhusu Bandari ya Mtwara, alisema gharama zinakuwa kubwa kwa sababu kuna umbali kidogo, hawana mzigo wa kutosha na meli hukosa shehena ya kurudi.

“Hatuongezi bei, lakini wadau wengine wanaangalia umbali na kurudisha faida yao. Tutaendelea kufanya maboresho kuhakikisha bandari inakuwa na meli wakati wote ambazo hazisubiri msimu wa korosho ili gharama zipungue,” alisema.

Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi TPA, Charles Ogare, alisema mradi wa uboreshaji gati namba moja hadi saba ulioanza Juni mwaka jana unagharimu Sh bilioni 336.7.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.