Jaji ataja sababu ukatili wa jinsia

Mtanzania - - Leo Ndani - NA MWANDISHI WETU - MWANZA

UNYANYASAJI wa uchumi dhidi ya wanawake ndani ya jamii unatajwa kusababishwa na uelewa mdogo wa jamii hasa kuhusu makosa ya jinai.

Hali hiyo imeelezwa kuchangia wanawake wengi vijijini kuendelea kufanyiwa vitendo vya ukatili wa ngono na kuporwa haki yao ya kumiliki ardhi za mila.

Kauli hiyo ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Agnes Bukuku wakati akizungumza na Jumuiya ya Wataalamu wa Sheria, Majaji, Mahakimu, Mawakili na wanazuoni wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania, Nyegezi, Mwanza.

Alikuwa akizungumza katika mahakama ya mfano (Moot Court) katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza na kuratibiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Africa (WiLDAF) na Chama cha Majaji Wanawake (TAWJA), kama sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia.

“Masuala ya ukatili siyo ya kufumbia macho, upo katika sehemu zote hata vyuoni kuna rushwa ya ngono.

“Maofisa wa serikali, hospitalini na mahakamani, TAWJA na WiLDA wameona waandae Moot Court chuoni hapa kuwaongezea uelewa wanafunzi wa sheria kuwaonyesha jinsi ya kuendesha kesi mahakamani,” alisema Bukuku.

Fatuma Kimwaga ambaye ni Mwanasheria wa TAWLA, alisema rushwa ya ngono hasa maeneo ya kazi na vyuoni inatajwa kuwa ni miongoni mwa vitendo vya unyanyasaji vinavyoitesa jamii.

Alisema hali hiyo ndiyo imekilazimu chama cha TAWJA na WiLDAF kuona umuhimu wa kuwaelimisha wanafunzi wa vyuo vikuu wajue namna mahakama zinavyofanyakazi na tafsiri za sheria.

“Vitendo vya ukatili vinalenga kudidimiza uchumi wa wanawake na watoto maana vipo katika nyanja mbalimbali ikiwamo kazini, nyumbani, kubakwa, vipigo na kusababisha athari kubwa kwenye familia na kuongeza umasikini,” alisema Kimwaga.

Mwanafunzi wa Kitivo cha Sheria katika chuo hicho, Brightness Shija alisema huenda mjadala huo wa sheria ukawa chachu kwao katika kupambana na changamoto za sheria na siyo kufanya uamuzi kwa msukumo wa hisia.

“Somo la leo tumeona jinsi unavyotakiwa kuendesha kesi, unavyotakiwa kusimama mahakamani, kujenga hoja kwa kutumia vifungu vya sheria na jinsi majaji au mahakimu wanavyotakiwa kutoa uamuzi wakiongozwa na sheria badala ya mihemko,” alisema mwanafunzi huyo.

Emmanuel Mtawa ambaye ni mwafunzi wa Sheria mwaka wa nne SAUT, alisema ingawa walikuwa wakifanya mafunzo kwa njia ya vitendo, Moot Court hiyo iliyofanywa na mahakimu na wanasheria wazoefu imewaongezea uelewa jinsi ya kuendesha kesi mahakamani.

Mkuu wa Kitivo cha Sheria chuoni hapo, Dk. Erasma Rutechura alisema: “Shughuli hiyo ya mahakama ya mfano imefanyika kwa mara ya kwanza chuoni hapo na ni sehemu ya mitihani kwa baadhi ya wanafunzi wa sheria wa mwaka wa pili, watatu na wa nne”.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akimsikiliza daktari bingwa wa uchunguzi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Dr. Msafiri Marijani, baada ya kuwasili katika viwanja vya Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar. Kulia kwa rais ni Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed akifuatiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.