Sukari si ugonjwa wa matajiri, tahadhari ni muhimu

Mtanzania - - Taharirimtazamo - Na MWANDISHI WETU

KATIKA kipindi cha mlongo mmoja hadi miwili iliyopita, magonjwa kama kisukari, shinikizo la juu la damu (presha) pamoja na saratani, yalikuwa yakidhaniwa kuwa ni magonjwa ya mataifa tajiri au yaliyoendelea tu.

Dhana hii ilitokana na kile kilichoaminika kuwa hayo ni magonjwa ya watu wenye fedha au matajiri kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kununua na kutumia vyakula vya mafuta na vya kusindika.

Pia hii iliaminika kuwa wanaokula hivyo ndiyo hula vizuri.

Sasa hivi, imedhihirika kuwa magonjwa hayo huwapata hata watu wa kawaida, ambao kwa mtazamo wako unaweza kusema hawapo katika makundi ya watu tajiri.

Hivyo basi, magonjwa hayo hayajabadilika na wala haina maana kwamba vipato vya watu kifedha ndivyo chanzo cha matatizo, bali ni mtindo wa maisha ya watu ndio uliobadilika, ulaji wa vyakula bila ya kuzingatia aina ya chakula na virutubisho vilivyomo ndani yake.

Pamoja na kwamba kutakuwa na sababu za magonjwa kujitokeza kutokana na kurithi au mtu kuzaliwa akiwa na ugonjwa husika mfano kisukari, lakini kwa hali ya sasa zipo kesi nyingi zinazosababishwa na mtindo wa maisha.

Hali ya ujauzito mara nyingi huambatana na maudhi madogo madogo pamoja na hatari ya kuugua baadhi ya magojwa ukilinganisha na mtu mwingine. Mfano, mjamzito anaweza kuugua uchafu wa mkojo (UTI), magonjwa ya tumbo na hata kupungukiwa damu kwa haraka zaidi ukilinganisha na asiye na ujauzito.

Hii ina maana kwamba, pamoja na maudhi mengine na usumbufu ambao hujitokeza baada ya kuwa mjamzito, endapo itatokea kukawa na ugonjwa basi hii itaongeza ugumu katika kuilea mimba na kumfanya mama azidi kuchoka mwili kabla ya siku za kujifungua kufika.

Kwa upande wa ugonjwa wa kisukari kuna nyakati hali inaweza ikawa ni tofauti na inavyotarajiwa. Mwanamke inawezekana alikuwa na tatizo la kisukari kabla ya ujauzito, kwa kawaida na kama alikuwa amegundua tatizo hilo mapema atakuwa ameonana na wataalamu na wamemuanzishia matibabu stahiki.

Mara baada ya kupata ujauzito, kuna uwezekano baadhi ya dalili na usumbufu uliokuwa unajitokeza pindi sukari inapopanda, dalili hizo zikapungua au akawa hazioni kabisa.

Maana yake ni kwamba yeye ataona kuwa tatizo la kisukari limepotea na hata akaanza kutozingatia matumizi ya dawa na ushauri aliopewa ili kutibu tatizo la kisukari.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.