Vyuo vya wananchi msingi wa maendeleo

Mtanzania - - Taharirimtazamo -

MAENDELEO ya binadamu ni dhana inayojulikana sana nchini kuwa ni pamoja na uhuru kwa watu, unasisitiza umuhimu wa kuwawezesha watu katika maeneo ya afya, umri wa kuishi, elimu na kipato.

Katika muongo uliopita, Tanzania imeshuhudia ukuaji mzuri wa Pato la Taifa wa kiwango cha wastani wa asilimia 7, ambapo hata hivyo kinyume cha matarajio ya wengi, ukuaji huo haukwenda sambamba na kupungua kwa umasikini, isipokuwa kwa maeneo machache.

Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu iliyotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ya mwaka 2014, inaonyesha kuwa ukuaji wa kiuchumi ulishindwa kuongeza uwezo wa wananchi walio wengi kuishi maisha bora.

Aidha, ripoti hiyo inaonyesha kuwa japokuwa ukuaji wa uchumi ni jambo muhimu linalohitajika bado mageuzi hayo hayakwenda sambamba na kutengeneza fursa za ajira, kukuza kipato pamoja na kuongeza huduma za jamii.

Serikali imekusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya watu walioelimika na kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Ili kufikia malengo hayo, Serikali imekuwa ikitekeleza sera mbalimbali ikiwemo Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 1995 pamoja na Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya 1996 na hivyo kuongeza wigo na fursa kwa watu kujielimisha.

Hata hivyo, katika kipindi hicho, changamoto mbalimbali zimejitokeza zikiwemo udhaifu katika mfumo wa elimu na mafunzo, uhaba wa walimu, uhaba wa zana, nyenzo na vifaa na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na changamoto katika ithibati na uthibiti wa ubora wa shule na vyuo.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imeandaliwa ili kutoa mwelekeo wa elimu na mafunzo nchini kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia na changamoto za elimu na mafunzo kitaifa, kikanda na kimataifa, ili kuongeza fursa, ufanisi na ubora wa elimu na mafunzo nchini.

Moja ya shabaha ya msingi ya mabadiliko ya sera hiyo ni pamoja na kuongeza mkazo na msukumo katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuimarisha maarifa na stadi kwa wananchi ili waondokane na ujinga, umasikini na maradhi na kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, anasema katika mwaka 2017/18 imefanya tathmini ya hali ya miundombinu katika vyuo vyote 55 vya Maendeleo ya Wananchi ili kubaini uchakavu wa miundombinu, vifaa, mitambo na upungufu wa watumishi katika vyuo hivyo.

Aidha, Prof. Ndalichako, anasema Serikali pia inafanya upembuzi yakinifu wa miundombinu ambapo taarifa hiyo itasaidia kufanyika kwa ukarabati wa ujenzi katika vyuo 20 vya maendeleo ya wananchi katika Awamu ya Kwanza.

“Katika mwaka 2017/18, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vimedahili jumla ya wanafunzi 5,050 na kuwapa mafunzo katika fani za upishi, kilimo na ufugaji, ufundi umeme wa majumbani, ufugaji samaki na nyuki, ususi na ufumaji, usindikaji wa vyakula na matunda, ushonaji, uchomeleaji vyuma, umakenika, kompyuta, useremala, uashi, utengenezaji mapambo na ujasiriamali,” anasema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu ambao ni Karibu Tanzania Organization, Master Card Foundation, Aflatoun na Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania, zimeweza kuandaa programu za Elimu Haina Mwisho na Mpira Fursa zilizolenga kutoa elimu ya stadi za maisha na ujasiriamali kwa wasichana nje ya mfumo na kufungua fursa ya ajira kwa mchezo wa mpira wa miguu.

Anaongeza kuwa kupitia miradi hiyo, kiasi cha Dola 100,000 zimetengwa kwa kipindi cha miaka minne (4) ambapo katika mwaka 2017/18 wasichana 569 wamepatiwa mafunzo katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

Waziri Ndalichako anaongeza kuwa katika Programu ya Mpira Fursa ambapo kiasi cha Pauni za Uingereza 550,000 zimetengwa kutumika kwa kipindi cha miaka minne (4), jumla ya wasichana 523 kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii 27 wamepata mafunzo ya kuwawezesha kushiriki katika mchezo wa mpira wa miguu.

Moja ya majukumu ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyosheheni wasomi wenye maamuzi katika sera, sheria, mikakati na mipango ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi katika kufikia maendeleo endelevu na kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 kwa kutengeneza ajira za kudumu ambazo zitaongeza uzalishaji na wigo wa kodi.

Ili kufikia malengo hayo, ni wajibu wa Serikali kubuni mikakati ya namna ya kuwafuatilia wahitimu kwa nia ya kupima kiwango cha taathira kilichofikiwa kutokana na mafunzo yanayotolewa vyuoni, matokeo ya upimaji huo yatatumika katika kurekebisha mitaala na kufikia mikakati ya utekelezaji.

Aidha, Prof. Ndalichako, anasema Serikali pia inafanya upembuzi yakinifu wa miundombinu ambapo taarifa hiyo itasaidia kufanyika kwa ukarabati wa ujenzi katika vyuo 20 vya maendeleo ya wananchi katika Awamu ya Kwanza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.