Waziri Nyongo amaliza utata umiliki mgodi Nyabayombe

Mtanzania - - Kanda - Na FREDRICK KATULANDA

NAIBU Waziri wa Madini, Stanislaus Nyongo ameurejesha kwa wamiliki halali mgodi mdogo wa dhahabu wa Nyabayombe katika Kijiji na Kata ya Lubili wilayani Misungwi ambao ulikuwa uporwe na watu wasio na leseni.

Mgodi huo wenye viwanja 16 ulisajiliwa kwa namba 3686 Mei 25, mwaka 2017 na wamiliki wake wakiwa ni wakazi 150 wa Kitongoji cha Nyabayombe walioungana na kuwa kikundi kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuungana wapatiwe eneo la uchimbaji.

Hivi karibuni, kuliibuka mgogoro wa nani mmiliki halali wa viwanja 16 hivyo baada ya kundi jingine lenye wanachama 33 likiongozwa na Philipas Kapesa, kuibuka na kudai ndiyo walikuwa wamiliki halali wa mgodi huo.

Ilielezwa kuwa Lupimo akishirikiana na wenzake, Ahmada Butwiga na Shija Lupimo waliunda kikundi kipya cha Mimi Coso baada ya kuwageuka wenzao baada ya kukaribishwa kwenye kikundi cha Nyabayombo.

Baada ya kuunda kikundi hicho kipya walidai wao ndiyo wamiliki halali, mgogoro ambao ulifika hadi wizarani.

Waziri Nyongo alitembelea mgodi huo Novemba 19, mwaka huu na kusema kusema baada ya kusikiliza pande zote mbili zilizokuwa zikivutana alibaini kuwa wamiliki halali ni Kikundi cha Nyabayombe ambao ndiyo walipewa leseni ya uchimbaji na siyo kikundi cha Mimi Coso.

“Serikali ilitoa leseni ya mgodi huu wenye viwanja 16 kwa kikundi cha Nyabayombe hivyo wamiliki wanaopaswa kuendelea na shughuli za uchimbaji hapa ni kikundi hicho na siyo vinginevyo…. mgogoro huu umemalizika,” alisema Nyongo.

Naibu waziri alisema kama Kapesa na wenzake wanataka kuchimba watengeneze kikundi na kufuata taratibu zinazotakiwa siyo kutaka kuwapindua wenzao na kupora mgodi wa wananchi waliopewa kwa halali na serikali.

Mwenyekiti wa Mgodi huo Ntuja Shitungulu, alisemakutokana na uamuzi wa waziri, wameanza shughuli za uchimbaji na wanatarajia kusaidia kutoa ajira za kudumu na muda kwa wanakijiji zaidi ya 1000.

Alisema kuanza kwa uzalishaji kutawawezesha kulipia mrabaha Serikalini, ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Misungwi ikiwa ni pamoja na Kodi ya mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Meneja wa Mgodi Kasanda Mnada, alisema katika kipindi cha mwanzo cha kuanza uzalishaji wao wameanza kukarabati barabara ya kijiji chao kurahisisha huduma ya usafiri kutokana na barabara hiyo kuwa kwenye hali mbaya.

Diwani wa Kata ya Lubili, Ngagizi Zozozo (CCM) alisema amefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kutatua mgogoro huo na kuwarejeshea wananchi wenyeji wa kijiji hicho mgodi wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.