Watoto waajiriwa kwa malipo ya ndama

Mtanzania - - Kanda - Na SAMWEL MWANGA

BAADHI ya watoto katika Wilaya ya Meatu hasa vijijini wamekuwa wakiajiriwa na familia za wafugaji kwa ujira wa kulipwa ndama mmoja kwa mwaka mmoja.

Watoto hao wa kiume ni wenye umri kati ya miaka minane hadi 10 ambao walipaswa kuwa shuleni lakini wamekuwa wakifanyishwa kazi ya kuchunga ng’ombe za wafugaji hasa wenye makundi makubwa ya mifugo.

MTANZANIA ilipotembelea vijiji vya Usiulize, Makao, Bukundi na Nkoma ilishuhudia baadhi ya watoto hao wakiwa wanachunga mifugo hiyo.

Jilala Mboje mkazi wa Kijiji cha Usiulize, alisema wapo baadhi ya watoto hao huamua kuacha masomo katika shule za msingi nakwenda kufanya kazi hiyo.

Alisema mkataba wake huwa ni malipo hayo ambayo hufanywa kati ya familia ya mtoto na mfugaji.

“Mbona hili ni jambo la kawaida, wapo baadhi ya watoto ambao wanaamua kuacha kwenda shule hasa wa shule ya msingi wanakwenda kuajiriwa kuchunga ng’ombe za wafugaji ambao ni matajiri halafu familia ya mtoto wanapewa ndama jike kila mwishoni mwa mwaka,”alisema.

Alisema pamoja na kupata ajira hiyo lakini watoto hao wamekuwa wakipigwa na waajiri wao hasa wanapopoteza mifugo wakiwa kazini au kuliwa na wanyama wa porini.

Makono Malonja mkazi wa Kijiji cha Nkoma, alisema mtoto aliyeajiriwa hutakiwa kuhamia katika familia ya mfugaji huku akihudumiwa mahitaji muhimu ya binadamu ambayo ni malazi, mavazi na chakula.

Alisema baadhi ya wazazi wanalazimika kuwaingiza watoto wao katika ajira hizo kutokana na ugumu wa maisha.

Hata hivyo alisema wapo watoto ambao huacha masomo kwa hiari yao na kwenda kufanya kazi hizo hasa kwenye maeneo ya mapori ambayo yako mbali na makazi ya watu kwa ajili ya kupata malisho ya kutosha ya mifugo.

Mkuu wa wilaya ya Meatu, Dk. Joseph Chilongani alipotafutwa kuzungumzia suala hilo hakupatikana.

Lakini ofisa mmoja ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alikiri kuwapo ajira hizo kwa baadhi ya vijiji.

Alisema idara inapambana nalo lakini akaitaka jamii katika maeneo hayo ibadilike na kuacha ukatili huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.