Wananchi walalamikiwa kutochangia miradi ya shule

Mtanzania - - Mkoa - Na ASHURA KAZINJA

UELEWA mdogo kwa baadhi ya wananchi kuhusu dhana ya elimu msingi bila malipo, imechangia kwa kiasi kikubwa shule nyingi hasa za vijijini, kukosa maendeleo.

Changamoto hiyo ilielezwa jana mkoani hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Serikali linaloshughulikia masuala ya elimu msingi liitwalo Dimata, Salum Wamaywa, wakati wa kongamano la kushirikisha jamii juu ya changamoto za sekta ya elimu na utatuzi wake kwa shule za msingi wilayani Mvomero.

Kongamano hilo liliandaliwa na Dimata kwa kushirikisha wananchi, wadau wa maendeleo na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Wamaywa alisema kwamba, katika tathmini iliyofanywa na taasisi hiyo katika kata sita za wilaya hiyo na kupitia miradi 21 ya shule za msingi, waligundua jinsi wananchi wasivyoshiriki shughuli za maendeleo shuleni kwa kuwa wanaamini Serikali inatekeleza kila kitu.

“Baada ya kubaini kuwa wananchi wengi wana uelewa mdogo juu ya sera hiyo, tuliamua kuja na mradi wa kutoa elimu ya utatuzi wa changamoto zilizoonekana kujitokeza katika elimu ya msingi bila malipo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uelewa wa dhana ya utawala bora na uwajibikaji katika utoaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

“Kwa mfano, Serikali ilipeleka fedha katika maeneo fulani, lakini miradi ile haikukamilika kwa wakati na tulipotaka kujua sababu ni nini, tukagundua tatizo ni wananchi kutoelewa juu ya umuhimu wao wa kushiriki shughuli za maendeleo shuleni,” alisema Wamaywa.

Kwa upande wao, wadau mbalimbali wa elimu wilayani humo akiwemo Zakaria Peter, walisema wanaamini tatizo si kushindwa kuelewa dhana ya elimu bure, bali miradi mingi ya miundombinu katika shule za msingi katika maeneo yao haimaliziki kwa sababu wananchi hawaichangii miradi hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali, alisema Serikali wilayani Mvomero, inaamini changamoto zinazoitawala sekta ya elimu wilayani humo, zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa ushirikiano kati ya wadau wa elimu, wananchi na Serikali yenyewe.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.