Shida huduma ya afya Mtwara sasa basi

Mtanzania - - Jamil Na Afya - Na NORA DAMIAN -ALIYEKUWA MTWARA

SERA ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), inaelekeza kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo kila kijiji kinatakiwa kuwa na zahanati na kwa kata kuwa na kituo cha afya.

Katika kutekeleza sera hiyo, Serikali imeendelea kujenga zahanati na vituo vya afya katika maeneo mbalimbali hasa kwenye halmashauri ili kufikia asilimia 25 ya mahitaji na asilimia 50 kwa zahanati ifikapo mwaka 2025.

Mkoa wa Mtwara umeendelea kutekeleza adhima hiyo ya Serikali ya kila kijiji kuwa na zahanati, kata kuwa na kituo cha afya na wilaya kuwa na hospitali.

Mkoa huo unakadiriwa kuwa na watu wapatao 1,356,802 huku wastani wa ongezeko la watu kwa mwaka likiwa ni asilimia 1.2. Kati ya watu hao 312,067 wanaishi mjini na watu 1,044,735 wanaishi vijijini.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, anasema ujenzi wa zahanati na vituo vya afya umesaidia kuboresha huduma za afya na kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu.

“Tulikofanya mapinduzi ni kwenye huduma za afya, kuna maboresho makubwa ya utoaji huduma za kitabibu, ukarabati na ujenzi wa zahanati, vituo na hospitali,”anasema Byakanwa.

Anasema kwa miaka mitatu (2015 2018), wamejenga zahanati 40, vituo vya afya 10 na upanuzi wa vituo vya afya 13 unaendelea katika hatua mbalimbali.

Kwa upande wa zahanati anasema zimeongezeka kutoka 166 mwaka 2015 hadi 179 Juni 2018 huku vituo vikiongezeka kutoka 17 hadi 21.

Anasema hospitali za wilaya zimeongezeka kutoka tatu mwaka 2015 hadi nne Juni 2018 na hospitali iliyoongezeka ni ya Wilaya ya Nanyumbu.

Mkuu huyo wa mkoa anasema pia Hospitali ya Wilaya ya Ligula imeimarishwa ambapo limejengwa jengo la kuhifadhia maiti na jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD).

Mkoa huo pia umeanza mchakato wa ujenzi wa hospitali za wilaya katika Halmashauri za Wilaya za Mtwara, Nanyamba Mji na Masasi ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mkoa ya Ligula.

Hadi kufikia Septemba mwaka huu, mkoa huo tayari umepokea Sh bilioni 1.5 kati ya Sh bilioni 4.5 zilizotengwa katika bajeti ya 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi huo.

Kwa upande wa waajiriwa wapya alisema wameongezeka kutoka 1,548 (2015) hadi 1,867 (2018).

Kwa upande wa vifo vitokanavyo na malaria alisema vimepungua kutoka 285 (2015) hadi 107 (Juni 2018).

“Mkoa umeimarisha mapambano dhidi ya malaria, tumefanikiwa kugawa kwa wananchi vyandarua 339,067 vyenye viatilifu bila malipo,”anasema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo, upuliziaji wa viatilifu vya kuangamiza mazalia ya mbu umefanyika katika halmashauri zote ambapo lita 5,880 zimetumika kupulizia viuadudu.

Kuhusu upatikanaji wa dawa za malaria anasema umeongezeka kutoka asilimia 45 hadi kufikia asilimia 99 katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za afya.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Newala, Mussa Chimae, anasema zahanati mpya zimejengwa katika maeneo ya Maputi, Ngongo, Indapendo na Mtoke.

Anasema pia wanaendelea na ujenzi wa vituo vya afya vitatu na kwamba katika Kituo cha Afya Kitangali wamejenga majengo manane kwa gharama ya Sh milioni 400.

Majengo hayo ambayo yako katika hatua za mwisho za ujenzi ni pamoja na wodi ya wazazi, maabara, jengo la upasuaji na la kuhifadhia maiti.

Mkurugenzi huyo anasema pia wametenga zaidi ya ekari 35 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, anasema sasa hivi umeongezeka kutoka asilimia 60 (2016) na kufikia asilimia 98.

“Maboresho yaliyofanywa katika sekta ya afya yameleta mafanikio makubwa na sasa hivi mwananchi akienda kituo chochote hawezi kukosa dawa,”anasema Chimae.

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara, wanaishukuru Serikali kwa ujenzi huo ambao utawarahishia upatikanaji wa huduma bora.

“Tulikuwa tunasafiri umbali mrefu kufuata huduma lakini ujenzi wa zahanati na vituo vya afya utatupunguzia kero hii,”anasema Sikujua Hassan mkazi wa Magomeni, Mtwara.

Mkazi mwingine wa Kitangali, Selemani Jumanne, anasema Serikali imetambua shida za wananchi wa hali ya chini na kuona umuhimu wa kuboresha huduma za afya.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.