Wenye virusi vya Ukimwi washauriwa kuanza dawa

Mtanzania - - Kanda - Na BEATRICE MOSSES

BAADHI ya wananchi mkoani Manyara waliojitangaza kwamba wanaishi na virusi vya Ukimwi, wamewataka wananchi katika wilaya za Simanjiro, Mbulu na Hanang’, Mkoa wa Manyara, waliogundulika kuwa na virusi vya maradhi hayo, waanze kutumia dawa za kufubaza Ukimwi.

Wito huo ulitolewa juzi mjini Babati katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani baada ya mwakilishi wa kikundi cha wanaoishi na virusi hivyo, Dada Lulu, kueleza jinsi anavyoishi na maradhi hayo kwa miaka 28 sasa.

“Mimi kwa sasa nina miaka 49, niligundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi miaka ya 1990 na sasa hivi nina zaidi ya miaka 20 na ninaishi tu vizuri, nafanya kazi zangu vizuri na niko ‘very smart’ sina shida.

“Kwa hiyo usijinyanyapae kwa kusema nikipata kirusi wataninyanyapaa bali kinachotakiwa ni kuwa na marafiki pamoja na kujichanganya.

“Ukiishi na virusi vya Ukimwi, punguza ngono, acha pombe, acha mawazo, kula vizuri kama mimi kwani tangu nilivyojitangaza kwamba nina maradhi hayo, ninaishi vizuri na nimekuwa na marafiki wengi na hawaninyanyapai.

“Kwa hiyo nawaomba waliogundulika kwamba wana maradhi hayo, waanze dawa mapema ili waweze kuishi maisha marefu,” alisema Lulu.

Katika risala ya Mratibu wa Kuthibiti Maambukizi ya Ukimwi, Mkoa wa Manyara, Anna Fisoo, alisema kiwango cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi kimeongezeka kutoka asilimia 1.5 hadi kufikia asilimia 2.3 mkoani Manyara. Alisema kwamba, kumekuwa na sababu mbalimbali zinazosababisha maambukizi kupanda zikiwamo kuongezeka kwa mwingiliano wa watu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabethi Kitundu, alisema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanatakiwa kuisaidia Serikali kutoa elimu ya kujikinga na maradhi hayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.