Kalemani: Hatutakurupuka kusaini mikataba ya biashara

Mtanzania - - Biashara - Na VERONICA SIMBA - MTWARA

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema Serikali itatumia muda mwingi ili kujiridhisha na manufaa ambayo Taifa litapata kabla ya kusaini mikataba mbalimbali ya sekta ya nishati, hususan ya mafuta na gesi.

Alitoa kauli hiyo Mtwara juzi, wakati akizungumza na uongozi wa kampuni ya kigeni ya mwekezaji, Maurel & Prom kutoka Ufaransa, wanaotafiti na kuchimba gesi eneo la Mnazi Bay.

Kalemani, alitoa msimamo huo wa Serikali baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa kampuni hiyo iliyowasilishwa na Makamu Mkurugenzi Mkuu, Elias Kilembe, ambayo pamoja na mambo mengine, waliomba Serikali iharakishe mchakato wa utiaji saini mikataba ya uwekezaji zaidi katika sekta husika, ambayo walikwisha kuwasilisha.

Alisema Serikali haikusudii kumchelewesha mwekezaji, bali kinachofanyika ni kujiridhisha hatua kwa hatua, namna Taifa litakavyonufaika.

“Tutatumia muda wa kutosha kujiridhisha, hata kama ni miaka 40, lazima mikataba iwe na manufaa. Huo ndio msimamo wa Serikali.

“Sisi tunapenda wawekezaji, tunataka waendelee kuwekeza ili tupate manufaa ya gesi na mafuta, lakini tusiibiwe,” alisema.

Aliutaka uongozi wa kampuni husika kuchukua hatua stahiki za makusudi na haraka katika kudhibiti changamoto ya maji ya bahari kusogea karibu zaidi na kisima cha gesi cha Mnazi Bay, hivyo kuwepo hofu ya maji hayo kuingia kwenye kisima husika.

Alipongeza ukamilishaji wa mfumo wa kuunganisha visima vyote vya gesi vya Mnazi Bay, hali ambayo alieleza itasaidia katika kuimarisha ukaguzi na udhibiti.

“Naagiza kuanzia sasa kila gesi inayotoka katika visima vilivyopo, ipite kwenye mfumo huu mpya ili ituwezeshe kujua ni kiasi gani imetoka na kiasi gani kilipwe,” alisema.

Akikagua mtambo wa kuchakata gesi wa Madimba, ulio chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), alipongeza kazi nzuri inayofanywa na shirika hilo na kuwataka waongeze bidii zaidi katika usimamiaji wa rasilimali hizo za mafuta na gesi kwa manufaa ya Watanzania.

Katika ziara hiyo, Kalemani alikagua utekelezaji wa miradi ya umeme iliyo chini ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika Mtaa wa Ufukoni na Mbae Mashariki, Manispaa ya Mtwara na kuwaagiza viongozi wa shirika hilo katika maeneo hayo, kuhakikisha wananchi wote waliolipia umeme wanaunganishiwa huduma hiyo ifikapo Desemba 20, mwaka huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.