Tabora FC, Twiga zatupwa nje Kombe la Shirikisho

Mtanzania - - Habari Za Michezo - Na DAMIAN MASYENENE - MWANZA

MABINGWA wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) Mkoa wa Mwanza, Twiga FC, imeshindwa kusonga mbele katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo, baada ya kupoteza mbele ya Homeboys.

Twiga FC waliokuwa wenyeji wa mchezo huo, uliopigwa katika Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza juzi, walifungwa mabao 2-0 na Homeboys ya mkoani Shinyanga.

Ushindi huo umeiwezesha Homeboys kusonga mbele ambapo katika hatua inayofuata itakutana na Ambassador FC ya Simiyu, Desemba 8, mwaka huu.

Katika mchezo mwingine wa michuano hiyo, Boko ya Shinyanga imeitupa nje timu ya Hawise FC ya Serengeti mkoani Mara baada ya kuchapwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Timu nyingine iliyosonga mbele ni Bariadi United ya Simiyu kwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kuichapa Tabora FC ya bao 1-0.

Kwa matokeo hayo, Boko ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa Nyamongo SC ya Mara, katika hatua inayofuata Desemba 8, mwaka huu, huku Bariadi United wakiwa wageni wa Stand Dortmund ya Singida.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.