Mwakyembe atoa neno sakata la Wambura

Mtanzania - - Burudani - Na ADAM MKWEPU -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema atakutana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupata maelezo ya kina kuhusu sakata la Makamu Rais wa shirikisho hilo, Michael Wambura, kabla ya kutoa mwongozo wa nini kifanyike.

Wambura juzi alitinga ofisi za TFF, jijini Dar es Salaam, baada ya Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa Kamati ya Maadili iliyomfungia maisha kutojihusisha na soka.

Hata hivyo, Wambura hakufanikiwa kuingia ndani ya ofisi hizo, baada ya kuzuiwa, hatua iliyomfanya afanye mkutano na waandishi wa habari nje.

Kabla ya kupitisha uamuzi wa kumfungia, Kamati ya Maadili ilimkuta Wambura na hatia katika makosa matatu, kupokea au kuchukua fedha za shirikisho za malipo ambayo hayakuwa halali kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanuni za maadili za TFF toleo la 2013.

Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya Kampuni ya Jeck System Limited huku akijua malipo hayo si halali, kinyume na kifungu cha 73(7) cha kanuni za maadili za TFF toleo la 2013.

Kosa la tatu ni kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho hilo, kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa mwaka 2015.

Lakini Aprili mwaka huu, Wambura alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga hukumu kabla ya Novemba 30, kushinda.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwakyembe, alisema wizara yake haiwezi kutoa mwongozo wa kile kinachopaswa kufanyika hadi pale itakapopata maelezo ya kina ikiwamo kupitia uamuzi wa Mahakama Kuu.

“Najiandaa kukutana na TFF ambao wao ndio wahusika wakuu watakaonipa maelezo kuhusu sakata hilo, lakini kabla ya hapo hakuna jambo ninalofahamu zaidi ya kusikia na kusoma kwenye magazeti.

“Baada ya kufahamu kila kitu nitakaa chini na jopo langu la wanasheria na jambo zuri binafsi ni mwanasheria, lakini nina washauri wa michezo hapa wizarani ambao tutakaa pamoja kabla ya kutoa mwongozo wa kitu gani kifanyike,” alisema Mwakyembe.

Uamuzi wa Mahakama Kuu una maana kwamba, Athumani Nyamlani ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya Makamu wa Rais baada ya Wambura anapaswa kuondoka katika ofisi za shirikisho hilo.

TIZI: Wachezaji wa timu ya Pamba SC ya Mwanza, wakifanya mazoezi katika Uwanja wa Nyamagana juzi kujiandaa na michezo ya Ligi Daraja la Kwanza. – PICHA: DAMIAN MASYENENE

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.