Shahidi: Malinzi aliikopesha TFF mamilioni

Mtanzania - - Burudani - Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mhasibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sereki Mesack, amedai mahakamani kwamba aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi, alilikopesha mamilioni ya fedha.

Sereki anadai haoni kama kuna tatizo katika stakabadhi zenye thamani ya Sh milioni 25 na Dola za Marekani 27,500, ambazo Jamal Malinzi alilikopesha shirikisho hilo.

Shahidi huyo wa tisa wa upande wa Jamhuri, alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, wakati akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Shadrack Kimaro, shahidi huyo alidai kazi yake ilikuwa kuingiza stakabadhi na nyaraka za malipo katika kompyuta.

Shahidi anadai Februari 9 mwaka 2016, Malinzi aliikopesha TFF Sh milioni 10, Mei 5/2016 aliikopesha Dola za Marekani 8,000 na tarehe hiyo hiyo aliikopesha TFF Dola za Marekani 7,000.

Alidai Mei 27,2016 Malinzi aliikopesha TFF Sh milioni tano kwa ajili ya timu ya Taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys, Juni 16 aliikopesha TFF, Dola za Marekani 10,000 Agosti 2, mwaka huo aliikopesha Dola za Marekani 1,000 kwa ajili ya kumwezesha Ayoub Nyenzi na Dk. Yunga kwenda Afrika Kusini.

Sereki anadai Septemba 21 mwaka huo, Malinzi aliikopesha TFF Sh milioni saba na tarehe hiyo hiyo aliikopesha Sh milioni tatu kwa ajili ya Serengeti Boys.

Alidai Septemba 22 mwaka huo, alikopesha shirikisho hilo Dola za Marekani 15,000 kwa ajili ya kuiwezesha Serengeti Boys kwenda Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Malinzi anawakilishwa na Wakili Richard Rweyongeza ambaye alitaka kujua kama anafahamu kuwa Malinzi anadaiwa kuiba fedha, hata hivyo shahidi huyo alijibu kuwa hizo tuhuma alizisikia baada ya kushtakiwa.

Rweyongeza alimhoji shahidi kwamba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa na wenzake watatu wanashtakiwa kumwezesha Malinzi kuiibia TFF, alitaka kujua kama anajua hilo, lakini shahidi alidai aliisikia baada ya kina Malinzi kushtakiwa na Takukuru.

Washtakiwa katika kesi hiyo mbali ya Malinzi (57), wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine (46) na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga (27).

Meneja wa TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Marekani 173,335 na Sh 43,100,000.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kutokaan na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha ambayo ni miongoni mwa mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana, huku wenzao Zayumba na Flora wapo nje kwa dhamana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.