DC aagizwa wadaiwa sugu waitwe mbele ya kamati ya ulinzi

Mtanzania - - Leo Ndani - Na FRANCIS GODWIN

MKUU wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdalah ameagiza wadaiwa sugu katika Chama cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa cha Mazombe Saccos Ltd, Ilula kuitwa mbele ya kamati ya ulinzi na usalama wilaya ili kueleza watakavyorejesha mikopo yao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alitoa agizo hilo juzi, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wanachama wa Mazombe Saccos ltd .

Alisema dhamira ya Serikali ni kuendelea kuweka misingi imara ya ushirika na kuona wanachama wake wananufaika na ushirika hivyo si vema kuona wanachama wachache wakijinufaisha kwa kukopa na kushindwa kurejesha mikopo yao.

“Mimi napenda kuona Mazombe Saccos Ltd, inakuwa imara zaidi na sipendi kuona wachache wanajinufaisha na pesa za wengine nashauri wote wanaodaiwa waitwe na mimi mnialike nitakuja na kamati yangu ya ulinzi na usalama ili wajieleze watalipaje madeni yao,” alisema.

Kuwa pamoja na mazuri mengi yanayofanywa na Mazombe Saccos kwa kuongoza kwa mkoa mzima kuwa Saccos ya kwanza kufanya vizuri ila madeni sugu yanahatarisha chama hicho.

Alitaka viongozi wa Mazombe Saccos Ltd kabla ya kutoa mikopo kwa wanachama wake kufika maeneo yao ili kukagua shughuli za kiuchumi ambavyo wameombea mikopo hiyo,badala ya kutoa mikopo kiholela .

“Sababu kubwa ya mikopo kutorejeshwa ni kutokana na baadhi yao kukopa pesa Saccos na kwenda kunywea pombe ama kufanyia starehe na mwisho wa siku kushindwa kurejesha mikopo hiyo,”alisema Asia.

Alipongeza mkakati wa kukusudia kujenga ghala la barafu la kuhifadhia nyanya kuwa litasaidia kumfanya mkulima wa nyanya Ilula kutoendelea kumwaga nyanya kutokana na kukosa soko.

Meneja wa Mazombe Saccos Ltd, Longino Ngwada alisema mkakati wa kupata fedha za ujenzi wa ghala hilo la kuhifadhia nyanya Ilula unaendelea kufanyika na awali waliandika andiko la kuomba ufadhili wa Sh milioni 400 ila wameshauliwa kuandika andiko la bilioni 1.5 ambalo limekamilika .

Akisoma taarifa yake kwa wanachama wa Mazombe Saccos Ltd, Mwenyekiti wa Bodi, Yohana Mwemutsi alisema tayari wamepata kukopesha zaidi ya bilioni 6 toka chama kilipo anzishwa na hali ya urejeshaji mikopo si mbaya sana.

Alisema ikopo iliyorejeshwa ni bilioni 5.7 kati ya 6.7 zilizokopeshwa, hku mikopo iliyopo nje ni Sh milioni 965.7 na mikopo chefuchefu ni Sh milioni 459.4.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.