Majaliwa azungumzia Tehama katika uwajibikaji

Mtanzania - - Leo Ndani - NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya Tehama ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kutumia vizuri teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi na kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.

Majaliwa alisema hayo katika sherehe za utoaji tuzo za mashindano ya Tehama ya HUAWEI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache. Ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo. Na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi,” alisema.

Alisema Serikali inaamini matumizi ya Tehama yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja.

“Matumizi ya Tehama kwa kiasi kikubwa yatapunguza gharamaza za uendeshaji kwani yanaweza kufanikisha mawasiliano binafsi, warsha na maelekezo mbalimbali kuwafikia walengwa bila ya kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.”

Alisema Juni 2017 Rais Dk. John Magufuli alizindua mfumo wa ukusanyaji Mapato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwa njia ya kielektroniki na kudhihirisha kuwa, sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni muhimili muhimu wa maendeleo kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, elimu, afya, kilimo, uvuvi na ufugaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.