Mengi akutana na wawekezaji kutoka China

Mtanzania - - Biashara - Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MWENYEKITI Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amekutana na wawekezaji kutoka China kwa ajili ya chakula cha mchana pamoja na kuwakaribisha washirikiane kufanya uwekezaji kwenye sekta mbalimbali nchini.

Dk. Mengi alifanya mazungumzo hayo juzi alipokutana na wawekezaji wakubwa 30 kutoka China kwa lengo la kuwahamasisha wawekezaji hao kuja kuwekeza nchini kwani kuna fursa nyingi.

Alitaja sekta kwa ajili ya uwekezaji kuwa ni pamoja na ujenzi wa bomba la gesi kutoa Dar es Salaam hadi Uganda, uchimbaji wa madini ya dhahabu, kukifufua kiwanda cha General Tyre cha mjini Arusha pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kubangulia korosho mkoani Mtwara.

“Ninawakaribisha Tanzania tufanye uwekezaji wa pamoja kwa sababu kuna fursa nyingi, ninawakaribisha tushirikiane katika ujenzi wa bomba la gesi, uchimbaji wa madini, ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho mkoani Arusha na ikiwezekana kukifufua kiwanda cha General Tyre, kama yupo mmoja kati yenu atakayehitaji namkaribisha” alisema Dk. Mengi.

Dk. Mengi alisema Mtwara korosho zinapatikana kwa wingi lakini kuna uhaba wa viwanda vya kubangulia korosho, aliwaomba kushirikiana naye katika ujenzi wa viwanda hivyo.

Aliwaeleza wawekezaji hao kuwa Tanzania kuna ardhi nzuri yenye rutuba, rasilimali nyingi pamoja na madini mbalimbali kama vile dhahabu, almasi, tanzanite na nyinginezo, hivyo aliwakaribisha wawekezaji hao kuungana naye katika kufanya uwekezaji.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini, Dk. Wang Ke, alisema Dk. Mengi ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa waliofanikiwa Tanzania na amekuwa akiwasaidia watu mbalimbali wasiojiweza.

Alisema Dk. Mengi ameleta mchango mkubwa kwenye sekta ya viwanda Tanzania kwa kujenga viwanda vingi na kuajiri watu wengi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.