Serikali: Tumeweka mazingira bora ya kufanya biashara

Mtanzania - - Biashara - Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora, amesema dhamira ya Serikali kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hapa nchini haiepukiki.

Akizungumza baada ya kikao cha kwanza cha Kamati ya Mazingira ya Biashara cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Profesa Kamuzora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisema wajumbe waliopo kwenye kamati hiyo ni mahiri na anategemea watatoa mapendekezo yanayolenga kulisaidia taifa.

“Lengo la kamati hii ni kuboresha mazingira ya kufanya biashara hapa nchini ili yaweze kuwa rafiki na kuchochea biashara na uwekezaji ambao utapunguza pia tatizo la ajira na kuchangia ukuaji kwa uchumi na maendeleo kwa ujumla,” alisema Profesa Kamuzora.

Alisema kamati itaandaa mpango kazi ambao utatoa mwongozo kwa upande wa sekta ya umma na binafsi katika utekelezaji wa mapendekezo ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia zaidi uwekezaji hapa nchini.

“Changamoto za kisera, sheria na uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali imekuwa ni sababu ya uanzishaji wa biashara au uwekezaji nchini kuwa mgumu, hivyo kamati ninayoisimamia itakwenda kutatua kero hizo kwa kuja na mapendekezo yatakayokuwa mwarobaini katika kuboresha mazingira ya biashara,” alisema.

Alisema ni vizuri kujitathmini kama mapendekezo yanachukuliwa hatua stahiki katika kuboresha hali ya ufanyaji biashara kwani kufanikiwa kwa kamati hiyo ndiyo kutazibeba kamati nyingine zote kutokana na mwingiliano wake na sekta nyingine.

“Tutafanya kazi kwa nguvu zetu zote katika eneo hili. Kuundwa kwa kamati hii chini ya TNBC kuna maana kubwa katika kuweka mazingira ya biashara vizuri kwa kuondoa vikwazo na changamoto inazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” alisema Profesa Kamuzora.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe, ambaye pia ni mjumbe katika kamati hiyo, alisema kamati hiyo itafanya kazi ambayo italeta matokeo chanya katika kuweka mazingira rafiki na bora katika kufanya biashara na kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.

“Mazingira ya uwekezaji nchini umekuwa mgumu kutokana na sheria mbalimbali za baadhi ya taasisi kukinzana na kuchangia kuzorota juhudi za kukuza uwekezaji nchini,” alisema Mwambe.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.