Ndanda waitangazia ubaya TZ Prisons

Mtanzania - - Burudani - Na ADAM MKWEPU -DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Ndanda FC, umeionya Tanzania Prisons kuwa isitegemee mteremko, wakati timu hizo zitakapokutana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa keshokutwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Ndanda FC ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 14, baada ya kucheza michezo 15, ikishinda mitatu, sare tano na kupoteza michezo saba.

Katika mchezo wa Ligi Kuu uliopita Ndanda FC ilipoteza dhidi ya Coastal Union baada ya kufungwa bao 1-0 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Wapinzani wao, Prisons wapo nafasi ya 19, wakiwa na pointi 10, baada ya kushuka dimbani mara 15, wakishinda mchezo mmoja, sare saba na kupoteza michezo saba.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Ndanda, Idrisa Bandali, alisema wamejifunza mambo mengi baada ya kupoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Coastal Union na sasa wanataka kutumia vema faida ya kucheza uwanja wa nyumbani kwa kuvuna pointi tatu dhidi ya Prisons.

“Wachezaji wote wapo tayari kupambana, lakini lazima tukiri kwamba hatukucheza vizuri mchezo uliopita kule Tanga.

“Benchi la ufundi lilibaini hilo na kuweka mkazo katika safu ya ushambuliaji kuhakikisha inatumia kwa umakini kila nafasi inayopatikana kufunga mabao, lakini pia katika eneo la ulinzi ambalo lilionekana kufanya makosa ya mara kwa mara ambayo ni hatari pale mnapokutana na timu yenye mastraika makini,” alisema Bandali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.