Coastal United waapa Mbeya City hawatachomoka salama

Mtanzania - - Burudani - Na RAHAHMA SWAI (TSJ) -DAR ES SALAAM

TIMU ya Coastal Union imetamba kuicharaza Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumapili Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Coastal Union ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 22, baada ya kushuka dimbani mara 14, ikishinda mitano, sare saba na kupoteza michezo miwili.

Katika mchezo uliopita, Coastal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Timu hiyo itakutana na Mbeya City ambayo katika mchezo wake wa mwisho ilishinda mabao 4-1 dhidi ya African Lyon Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mbeya City baada ya ushindi huo ilichumpa hadi nafasi ya tano, baada ya kujikusanyia pointi 22, ilizozipata baada ya kushuka dimbani mara 15, ikishinda michezo sita, sare nne na kufungwa michezo mitano.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda, alisema licha ya kwamba wanawaheshimu wapinzani wao, lakini hawatatoka lengo ni kutafuta pointi tatu muhimu.

“Tunaendelea vizuri na maandalizi, tukiamini tunaenda kucheza na timu bora na ambayo ipo kwenye mashindano kwa ajili ya kushindana na ina wachezaji wenye uzoefu.

“Tunatarajia mchezo wenye ushindani, lakini tupo tayari kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza mbele yetu,” alisema Mgunda.

“Majeruhi ni jambo lingine ambalo linaweza kutukwamisha safari yetu, hivyo tunawaomba mashabiki waendelee kuiombea timu yao, pia waje kushangilia ili kuongeza morali ya wachezaji waweze kujituma na timu kupata matokeo mazuri,” alisema Mgunda.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.