Polisi wa dhahabu wafukuzwa kazi

Wafikishwa mahakamani kwa rushwa, uhujumu uchumi

Mtanzania - - Mbele - BENJAMIN MASESE NA FATUMA SAID

JESHI la Polisi limewasimamisha askari wanane wenye vyeo mbalimbali kwa kutenda makosa kinyume na mwenendo wa kiutumishi ndani ya jeshi hilo, pia wamefikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka 12 yanayowakabili.

Askari waliosimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani ni E. 4948 CPL Dani Kasala, F. 1331 CPL Matete Misana, G.1876 PC Japhet Lukiko, G.5080 PC Maingu Sorrah, G.6885 PC Alex Nkali, G.7244 PC Timoth Paul na H.4060 PC David Ngelela.

Pia aliyekuwa Kiongozi Mwandamizi wa Mkoa wa Mwanza, SSP Moris Okinda, aliyeongoza kikosi kilichoomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 700, naye amesimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.

Mbali na askari hao, watuhumiwa wengine katika sakata hilo waliofikishwa mahakamani ni Sajid Hassan (28) ambaye ni mkazi wa Ilala, Dar es Salaam na Mwanza, Kisabo Kija maarufu kwa jina la Mkinda (55) mkazi wa Geita, Emmenuel Ntemi (63) ambaye ni dereva na mkazi wa Kijiji cha Mwatulole na Hassan Sajiq Hassan (28) ambaye ni raia wa Pakistan na mkazi wa Mwanza pia ni mfanyakazi wa duka la kuuza vito.

Kitendo cha askari hao kuchukuliwa hatua ya kusimamishwa kazi, kimetokana na tukio la kukamatwa kwa watuhumiwa watatu waliokuwa na dhahabu kilo 323.6 zinazodaiwa kuwa na thamani zaidi ya Sh bilioni 27.18 na Sh milioni 305 eneo la Kivuko cha Busisi mkoani Mwanza na kufanya makubaliano ya kuomba rushwa ili kuwasindikiza.

MAHAKAMANI

Wakisomewa mashtaka jana na Mwanasheria wa Serikali, Castus Ndamgoba kwa kusaidiana na wenzake watatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza mbele ya Hakimu Gwai Sumaye, alidai watuhumiwa hao 12 wanakabiliwa na makosa 12 yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Makosa mengine ni utakatishaji fedha haramu, kuomba na kupokea rushwa, kushawishi, kuisababishia hasara Serikali, kushiriki vitendo vya rushwa, uhalifu wa kupanga, kumiliki madini kinyume na sheria, kutakatisha fedha haramu, kufanya biashara ya madini kinyume na sheria na kuandaa mpango wa makusudi kutenda vitendo vya rushwa.

Akiwasomea kila mmoja makosa yake, Wakili Ndamgabo, akisaidiana na mawakili wenzake wa Serikali wakiwamo Robert Kidando na Jacqueline Nyantori, alidai kosa la kwanza ambalo ni la uhujumu uchumi linawahusu washtakiwa wanne ambao ni wafanyabiashara Sajid, Kisabo, Kija na Hassan.

Ndamgabo alidai washtakiwa hao waliongoza na kupanga uhalifu kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2002 kwamba kati ya Desemba 15, 2018 na Januari, 2019 mwaka huu katika maeneo tofauti ya miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Kagera na nchini Rwanda kwa pamoja wakishirikiana na watumishi wa umma kwa makusudi au kwa kutokujua, waliwezesha fedha za biashara ya uhalifu.

Kosa la pili linawahusu mshtakiwa wa tano hadi wa 12 ambao ni Okinda, Kasala, Misana, Alex, Maingu, Japheth, Timoth na Kadama.

Kosa la tatu ni kumiliki madini hayo bila kibali na kinyume cha sheria ya madini ya mwaka 2014, linamhusu mshtakiwa wa kwanza Sajid ambaye alikamatwa akiwa na kilo 319.59 za dhahabu.

Kosa la nne linalowakabili washtakiwa namba tano hadi 12 ambalo ni la vitendo vya rushwa ambavyo ni kinyume na sheria ya kupambana na kuzuia rushwa namba 11 ya mwaka 2011 kwamba Januari 4 na 5, mwaka huu katika Kivuko cha Kigongo wilayani Misungwi, Busisi na Kamanga wilayani Sengerema, walipokea rushwa ya Sh milioni 700 kutoka kwa washtakiwa wa kwanza hadi wa nne.

Mwendesha mashtaka huyo alizidi kuieleza mahakama kuwa kosa la tano linawahusu mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne siku hiyo hiyo wakidaiwa kutoa rushwa ya Sh milioni 700 kwa SSP Okinda na askari wenzake zikiwa ni ushawishi ili wasimkamate Sajid aliyekutwa akiwa na dhahabu hiyo.

Kosa la sita pia ni la mashtaka ya rushwa linalowakabili washtakiwa wa tano hadi wa 12 wanaodaiwa kuwa Januari 4 hadi 5, mwaka huu katika eneo la Kigongo Misungwi na Busisi Sengerema wote walishawishi na kujaribu kupokea rushwa ya Sh milioni 300 ili wasimkamate mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Abdallah na kumfikisha katika vyombo vya sheria baada ya kumkuta akiwa na madini hayo.

Shtaka la nane ni kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.89, linawakabili mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne kutokana na matendo yao kwa makusudi kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.

Kosa la tisa ni kutakatisha fedha haramu kinyume cha sheria ya mwaka 2006 na sheria ya uhujumu uchumi kwa kumiliki na kufanya biashara ya madini, linawakabili mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne baada ya Abdallah kukutwa akimiliki madini kilo 319.59 na kufanya biashara ya madini kinyume cha sheria.

Shtaka la 10 linawaangukia washtakiwa wote kwa pamoja walijihusisha na miamala ya dola 11,747,377.46 za Marekani katika maeneo tofauti tofauti ikiwa ni kosa la uhalifu wa kupanga kinyume cha sheria ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Mashtaka ya 11 na 12 ni ya kutakatisha fedha ambapo kosa la 11 linalowahusu washtakiwa wote ni tangulizi la tendo la rushwa na utakatishaji fedha haramu ambalo ni kinyume cha sheria namba 12 ya mwaka 2006 pamoja na sheria ya uhujumu uchumi kwamba washtakiwa namba tano hadi 12 walijipatia Sh milioni 700 kutoka kwa washtakiwa wa kwanza hadi wa nne.

Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya uhujumu uchumi na kesi hiyo namba 1/2019 iliahirishwa hadi Januari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena. Washtakiwa hao walipelekwa katika Gereza la Butimba.

DCI

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, alisema kazi iliyofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola tangu Januari 5, mwaka huu ni kubwa na imesababisha watuhumiwa 12 kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Alisema vitendo hivyo ni haramu na kamwe jeshi hilo halitaweza kuvumilia kikundi cha namna hiyo huku akiwapongeza waliotoa taarifa za siri kufanikisha suala la kukamatwa kwa dhahabu hiyo.

“Fedha hizo zingeweza kununua dawa ngapi au zingeweza kutengeneza madawati mangapi, lakini kikundi cha watu wachache kilitaka kujinufaisha wenyewe ili wengine wateseke, wito wangu kwa Watanzania kila mmoja ashiriki vita vya uhujumu uchumi.

“Sote tunatambua vita ya uchumi ni ngumu na hatarishi lakini tunasema tutapambana hadi mwisho na polisi hatulei rushwa,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.