Watanzania kuajiriwa kiwanda cha kutengeneza pikipiki

Mtanzania - - Habari - Na DEUS MHAGALE -DAR ES SALAAM

Anayenunua pikipiki kwetu hatopata tabu ya kutafuta vifaa kwa kuwa vitakuwa vinapatikana nchini - Raymond Huang

KAMPUNI ya Whuzho Investment inakusudia kuajiri wafanyakazi 200 ifikapo mwaka 2020 kwa lengo la kuinua uchumi.

Kampuni hiyo ya kutengeneza pikipiki aina ya Hon LG iliyosajiliwa nchini, inatarajia kuajiri Watanzania baada ya kupata kibali cha kufungua kiwanda cha kuunganisha pikipiki kilichopo eneo la Kisemvule, wilayani Mkuranga.

Meneja wa kampuni hiyo, Raymond Huang, alisema pamoja na kutoa ajira hizo pia ina lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuinua uchumi wa viwanda.

“Tumejipanga kuajiri wafanyakazi 200 hadi ifikapo mwaka 2020, kwa sasa tuna jumla ya watumishi 120 na kati ya hao, 95 wana ajira rasmi na 25 ni vibarua,” alisema.

Pia alisema kampuni hiyo imeshathibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hivyo wana imani watakidhi mahitaji ya Watanzania.

“Kabla ya kufungua kampuni tulikuwa tukiagiza pikipiki kutoka nchini China kwa zaidi ya miaka saba hadi ilipofika mwaka 2016 ndipo tukaamua kusajili kampuni yetu na sasa tumekubaliwa baada ya kuonekana tunafaa kulingana na ubora wetu,” alisema Huang.

Alisema mitambo ya kisasa iliyopo katika kampuni hiyo inafanya wataalamu kutengeneza pikipiki za uhakika kulingana na mazingira yaliyopo nchini.

Alisema kiwanda hicho pia kitauza vifaa vya pikipiki ili kuondoa usumbufu uliopo wa upatikanaji wa bidhaa hizo pindi pikipiki zinapoharibika.

“Anayenunua pikipiki kwetu hatopata tabu ya kutafuta vifaa kwa sababu vitakuwa vinapatikana nchini badala ya kusubiri kuagiza China,” alisema.

Alisema kiwanda hicho kimejipanga kufanya kazi karibu na wajasiriamali wadogo na kutatua changamoto walizonazo ili kuhakikisha Tanzania inapaa juu kiuchumi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.