Viboko wavamia bwawa Mugumu, waharibu mfumo wa umeme

Mtanzania - - Habari - Na MALIMA LUBASHA - SERENGETI

VIBOKO wawili kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wamevamia Bwawa la Manchira na kuharibu mfumo wa umeme wa pampu ya kusukumia maji na kusababisha huduma hiyo kukosekana kwa wiki moja sasa.

Akizungumza mjini hapa jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamsini, alisema wanyama hao walivamia bwawa hilo na kuharibu miundombinu na kusababisha wakazi 40,000 kukosa huduma hiyo.

Alisema tayari wametoa taarifa idara ya wanyamapori ili kuwawinda viboko hao na kuwaondoa ndani ya bwawa hilo na wameshanunua vifaa vingine kwa ajili ya kufanya marekebisho.

Alisema tangu Januari 5, mwaka huu wananchi wa Mugumu na vitongoji vyake hawana huduma ya maji kwa sababu ya uharibifu huo baada ya viboko hao kukata nyaya zinazotoa umeme katika transfoma kwenda katika pampu ambayo ni chanzo kikuu cha maji katika mji huo.

“Hii ni mara ya pili viboko hao kukata kata nyaya ambazo haziwezi kuunganishwa tena kiasi kwamba nimelazimika kuwatuma wataalamu wa maji kwenda Mwanza kufuata nyaya mpya,” alisema Hamsini.

Naye Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mugumu (Muguwasa), Charles Musiba, alisema ununuzi wa nyaya mpya utagharimu Sh milioni nane na itachukua siku nne kuzifunga ili huduma iweze kurejea.

“Hivi sasa akina mama na watoto wanatembea huku na huku kutafuta maji katika visima vya asili ambapo vijana wanaouza maji dumu lenye lita 20 kwa shilingi 500 na baadhi ya familia wanatumia zaidi ya shilingi 5,000 kila siku kwa mahitaji ya nyumbani,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.