JPM umeonesha mfano wa kuigwa

Mtanzania - - Tahariri -

RAIS Dk. John Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuzipaka rangi ndege mbili kati ya tatu zinazotumiwa na Rais ili zitumiwe na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kusafirishia abiria.

Kauli hiyo aliitoa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam juzi wakati akipokea ndege mpya ya sita aina ya Airbus A220-300.

Rais Magufuli alisema ndege hizo ambazo ni Fokker 28 na Fokker 50, zilizonunuliwa kwa matumizi ya Rais, zinapaswa kuungana na nyingine sita zilizopo kusafirisha abiria maeneo mbalimbali.

Uamuzi huo ni mfano wa kuigwa kwa watu wote waliopewa au watakaopewa dhamana ya uongozi katika taifa hili.

Sisi MTANZANIA Jumapili tunautafsiri uamuzi huo wa Rais Magufuli kwamba una maana pana na funzo kubwa la uzalendo kwa wananchi.

Tunaamini kwamba mojawapo ya ishara za mtu kuwa mzalendo kutoka kwenye uvungu wa moyo wake ni uamuzi mgumu kama huo, ambao si rahisi au haujazoeleka masikioni na machoni mwa watu.

Kupitia uamuzi huo wa Rais Magufuli, ile dhamira yake ya kulifufua na kuiimarisha ATCL imezidi kujidhihirisha na kujiweka kando na mitazamo ya kisiasa.

Tuanamuunga mkono kwa uamuzi wa kuziachia ndege hizo mbili za ofisi yake kwenda kusaidia usafirishaji wa abiria.

Hii ina maana kwamba usafirishaji wa abiria kupitia sekta ya anga utaimarika zaidi.

Pia ni tumaini letu kwamba kupitia uwapo wa ndege nyingi za kusafirisha abiria, sekta nyingine nazo zitarahisishiwa utendaji wake.

Kwa muktadha huo, ni wajibu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia ATCL kuzitunza ndege hizo kwa uhai wa biashara ya usafirishaji abiria ndani na nje ya nchi.

Pia ATCL wasiuangushe uzalendo wa Rais katika kuboresha sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.

Kutokana na hilo hawana budi kuendesha biashara hiyo kwa faida na kusaidia malengo ya Serikali ya kupanua wigo wa kukusanya mapato kupitia sekta hiyo.

ATCL wasiishie tu kuwa na idadi kubwa ya ndege bali wanatakiwa kuweka huduma bora katika shughuli za kila siku kwa msingi wa kuwa na viwango shindani kama ilivyo kwa makampuni makubwa yanayofanya biashara hiyo katika mataifa mengine.

Rais Magufuli kaonesha uzalendo namba moja katika biashara ya usafiri wa anga, ni matumaini yetu watendaji wa ATCL kwa weledi wa hali ya juu wataendesha shughuli zote za shirika hilo kwa uzalendo wa hali ya juu ili faida ya biashara hiyo ianze kuonekana mapema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.