Ubunge 2020 mwiba kwa wateule wa JPM

la Dk. Bashiru laashiria mwisho wa viongozi wanaocheza rafu

Mtanzania - - Mbele - Na EVANS MAGEGE - DAR ES SALAAM

MAANDALIZI ya kutafuta majimbo ya kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 yanaonekana kupata kikwazo kwa baadhi ya viongozi wa Serikali.

Hali hiyo inatokana na onyo lililotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, aliyewataka viongozi hao kuacha mara moja mikakati hiyo wakati bado ni watumishi wa umma na aliwashauri waridhike na nafasi walizoteuliwa na Rais Dk. John Magufuli.

Viongozi walionyoshewa kidole na Dk. Bashiru ni wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa mashirika ya umma walioanza kujipitisha katika baadhi ya majimbo kimkakati, kuendesha kampeni za chinichini kutafuta uungwaji mkono wa kugombea ubunge.

Akizungumza wiki iliyopita na wananchi wa Kijiji cha Lagangabilili kilichopo Itilima mkoani Simiyu, Dk. Bashiru alisema viongozi wengine wameanza kutembea na wagombea wanaowataka na kuanza kuwapigia kampeni za chinichini.

Onyo hilo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanatalitafsiri kama mbinyo wa kinidhamu utakaowashughulikia viongozi wenye tabia za kucheza rafu za kisiasa nyakati za uchaguzi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alipozungumza na gazeti hili, alisema Dk. Bashiru alitoa kauli hiyo kama ofisa mkuu wa nidhamu ndani ya chama tawala.

Kwamba ni wajibu wake kutoa kauli kama hiyo kama ilivyo kwa viongozi wa dini ambao kila siku lazima wawakumbushe waumini kutenda wema.

Alisema kipindi kilichopita watu walicheza rafu nyingi, walianza kujipitisha kabla ya muda kufika na watumishi wa umma wana maadili na miiko yao ni lini wanaweza kwenda kugombea nafasi za kisiasa.

“Sasa kama wanakwenda kinyume na taratibu hizo lazima wakemewe,” alisema Dk. Bana.

Pia alisema watu wakiachwa wakaendelea na siasa za chinichini

na ukifika muda uliopangwa hakutakuwa na mazingira sawa ya kisiasa.

“Hivyo onyo hilo la Dk. Bashiru linasaidia kuwabana hata wale wanaotamani nao kuanza kampeni za chinichini mapema.

“Uongozi wa sasa wa CCM ni kiboko, wacheza rafu za kisiasa wengi watakuwa wamenyooshwa na kamati ya nidhamu,” alisema.

Dk. Bana alisema ubunge wa mwaka 2020 hautakwenda kimazoea, kutokana na hulka ya Magufuli na Bashiru ambao wanapenda kufuata utaratibu.

Alisema kwa mazingira yalivyo hadhani kama watumishi wa umma watakimbilia kuwania ubunge kwa sababu inawezekana wakakosa kote.

“Kwa ninavyoona safu ya wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa,

makatibu tawala na wakurugenzi inaakisi lengo la CCM kuandaa viongozi, hivyo sioni kama ni rahisi kwa viongozi kujifanya hawatambui hilo labda kwa baadhi.

“Umeona kabisa watumishi wa umma matumbo joto, hii inaonesha wanamwamini Rais, ndiyo maana Rais kataka wajiamini sio kila maamuzi kusema yanatoka juu.

“Kwa msingi huu ninachokiona kutakuwa na watumishi wachache watakaothubutu kuacha nafasi zao na kwenda kugombea ubunge, haitakuwa watumishi wengi kama tulivyoshuhudia katika Serikali iliyopita,” alisema.

Pia alisema watumishi watakaothubutu kuacha nafasi zao na kugombea ubunge inawezekana ni wale wenye taaluma zao na hata wakikosa kote watapata kazi mahali pengine kulingana na elimu walizonazo.

“Lakini ile hamasa ya kukimbilia kwenye uchaguzi, watu wanaogopa kuwa hata waziri maana wanaogopa kutumbuliwa kwa fedheha kama ilivyowatokea baadhi wa mawaziri, na hii inatokana na haiba ya kiongozi tuliyenaye ambaye hapendi mchezo katika kazi,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala, alisema onyo la Bashiru linawakumbusha si tu watumishi wa umma bali makada wote wa CCM kuheshimu kanuni na sheria zinavyoelekeza.

Alisema watumishi wa umma hawatakiwi kujishughulisha na masuala ya siasa, lakini hawazuiliwi kugombea kwa kufuata utaratibu wa kujiuzulu nyadhifa zao kwanza.

“Dk. Bashiru anafanya vyema kuwa mkali dhidi ya watumishi wa umma walioanza kampeni za chinichini, bila kufanya hivyo hawa watu hawatafanya kazi na badala yake kuhangaika na mambo yao ya kisiasa, pia kujenga na kuimarisha mirija ya rushwa kuelekea katika uchaguzi mwakani,” alisema Profesa Mpangala.

Naye Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Profesa Mwesiga Baregu, alisema onyo hilo la Dk. Bashiru linaakisi ule mtazamo wa chama dola kwa maana ya kwamba mamlaka ya chama ndiyo ya Serikali.

“Mamlaka ya Serikali ya kikatiba yanachanganywa kwa sababu watumishi wa umma si wanachama wa CCM kikatiba, hivyo Dk. Bashiru anawaonya kama nani?” alihoji.

Alisema mteuliwa akishateuliwa kutoka katika chama hicho na kuwa mtumishi wa umma ina maana analipwa mshahara na Serikali na si chama.

“Dk. Bashiru anaweza kusimamia utendaji wa watumishi wa umma kupitia kwa mwenyekiti wake ambaye kaunganishwa nao moja kwa moja kikatiba.

“Lakini kwa mtazamo mwingine labda Dk. Bashiru awakemee kama wanachama wa CCM kwa maana ya kuwaeleza taratibu za chama zilivyo, lakini si kwamba ya kuwakemea kama RC, katibu tawala, mkuu wa wilaya au mkurugenzi kwa sababu hawa wana mamlaka zao zinazotambulika katika katiba,” alisema.

Pia alisema onyo la Dk. Bashiru linatokana na changamoto ya watumishi wa umma kuteuliwa kwa misingi ya chama chao na si kwa weledi wa mtu.

Alisema inavyoonekana kwa CCM ni tatizo kubwa la watu kuanza kampeni za chini chini na hiyo inatokana na kwamba wateuliwa wengi hawajiamini katika nafasi zao kwa sababu wanaweza kutumbuliwa wakati wowote.

“Lakini hata wakikimbilia kuchaguliwa nako wanaweza wakakuta mlango umeishafungwa, ndiyo maana nasema inaweza kuwa ngumu kwao,” alisema.

SHEREHE: Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (katikati), Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (wa tatu kushoto), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) na viongozi wengine wakifuatilia sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar jana. PICHA: IKULU ZANZIBAR

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.