Ummy: Elimu itaepusha mimba za utotoni

Mtanzania - - Habari - Na AMINA OMARI -TANGA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema ili kupunguza tatizo la mimba pamoja na ndoa za utotoni, wazazi hawana budi kuhakikisha wanawapeleka shule watoto wa kike.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati akitoa msaada wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule tano za sekondari zilizoko Jiji la Tanga.

Alisema elimu pekee ndiyo itaweza kusaidia kuwaepusha watoto wa kike na changamoto mbalimbali za masuala ya afya ikiwamo mimba za utotoni na namna nzuri ya kulea familia yake.

“Hawa watoto mkiwaacha wasome mpaka kidato cha nne wataweza kujua masuala ya lishe, watajua changamoto nyingi za kiafya na jinsi ya kukabiliana nazo kwa usahihi,” alisema Waziri Ummy.

Alisema tafiti za kiafya zinaonyesha kuwa kiwango cha elimu cha mama kinahusika kwa kiasi kikubwa katika malezi bora ya mtoto mchanga, hivyo ni jukumu la jamii kuachana na vitendo vya kukatisha masomo kwa watoto wa kike.

“Ukiangalia takwimu za chanjo mara nyingi utakuta mama ambao wana elimu ndogo ndio wanaongoza kwa kukatisha chanjo kwa watoto wadogo tofauti na mama mwenye elimu,” alibainisha Waziri huyo.

Hata hivyo, aliowaomba wadau wa maendeleo jijini humo kuhakikisha wanachangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kupunguza uhaba uliopo kwa sasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobiasi Mwilapwa, alisema kuwa ufaulu mkubwa wa wanafunzi umesababisha kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa katika jiji hilo.

“Mwaka 2018 wanafunzi 5,332 waliweza kufaulu na kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza, lakini mwaka huu wanafunzi 6,029 wameweza kufaulu kwenda sekondari hivyo ongezeko hilo la wanafunzi haliendani na miundombinu ya madarasa yaliyopo,” alisema DC Mwilapwa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji, alisema wana uhaba wa vyumba 71 vya madarasa katika shule za sekondari hivyo anaamini kuwa kukamilika kwa wakati kwa madarasa hayo kutawezesha kusaidia watoto wote waliofaulu kuhudhuria masomo yao.

Waziri Ummy ametoa matofali 3,500 pamoja na mifuko 250 ya saruji kwa shule tano za sekondari zilizoko katika Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

CHETI: Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Msasalaga (kulia), akimkabidhi cheti cha ubora Meneja Miradi wa Kampuni ya Wu Zhou Investment, Raymond Huang, katika hafla ya utoaji vyeti kwa kampuni zilizokidhi viwango vya ubora Dar es Salaam jana. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Biashara wa kampuni hiyo, Inocent Losha na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Viwanda ya TBS, David Ndebalema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.