DC Sikonge aonya uuzaji dawa zilizoisha muda

Mtanzania - - Habari - Na ALLAN VICENT -SIKONGE

MKUU wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wasio waaminifu wanaouza dawa za binadamu zilizoisha muda wake na kuwataka kuacha tabia hiyo.

Onyo hilo alilitoa juzi alipozungumza na madaktari na wauguzi wa hospitali teule ya wilaya hiyo na aliagiza kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa maduka yote yanayouza dawa baridi za binadamu.

Magiri alisema kuuza dawa zilizoisha muda wake ni kosa la jinai kwa sababu mtu akizinunua pasipo kujua na kuzitumia madhara yake ni makubwa na anaweza kupoteza maisha.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka ya dawa wamekuwa wakifanya tabia za udanganyifu na kuendeleza mchezo wa kuziuza licha ya kutambua kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Pia alionya yeyote atakayebainika kufanya mchezo huo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa dawa nyingine zikiisha muda wake zinakuwa sumu. Katika hatua nyingine, aliwataka waganga wakuu wa hospitali, vituo vya afya na zahanati zote wilayani humo kuhakikisha dawa zilizopo katika stoo zao ni zile zinazofaa kwa matumizi ya binadamu na wakibaini kuwa hazifai tena watoe taarifa ili ziteketezwe haraka iwezekanavyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.