Bunge ‘limeuza na kununua mgogoro’

Mtanzania - - Jichopevu - Na MARKUS MPANGALA

MJADALA mzito unaendelea nchini kuhusiana na sakata la Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa wito kupitia vyombo vya habari kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka chini ya Uenyekiti wa Kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka, ifikapo Januari 21, mwaka huu. Baada ya kuona Bunge limeshutumiwa kumwita ‘kihuni’ CAG, Alhamisi wiki hii taifa lilijulishwa kuwa limepeleka wito wa kimaandishi kwa CAG kumtaka ajitokeze mbele ya Kamati tajwa.

Mjadala huo pia umehusisha juu ya taratibu, kanuni, sheria na katiba ya nchi yetu. Makundi mbalimbali yamehoji uamuzi wa Spika kumwita CAG, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Je, ni halali Bunge kumwita CAG? Bunge linaweza kumwita mtu yeyote kumhoji kwa mujibu wa Sheria ya Haki na Kinga ya Bunge: The Parliamentary Immunity, Powers, and Privileges ACT, Namba 3 ya 1998, Kifungu cha 18-20.

Katika kifungu hicho kunaelezwa kama ifuatavyo: “Bunge au Kamati inaweza kuamrisha mtu yeyote kufika mbele ya bunge au kamati ili kutoa ushahidi, au nyaraka yoyote juu ya jambo fulani.”

Hata hivyo duru za kisheria zinasema kuwa sheria zina matabaka. Kwamba zipo sheria zinazolingana na kuna zinazozidiana. Kwenye Sheria kuna kanuni ya ‘The repugnant to or inconsistent with parent Act”, inayotumika kuainisha matabaka ya kisheria.

Mathalani, mkataba wa Muungano unaelezwa kuwa uko juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar. Kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar zina hadhi sawa kwenye mambo yasiyo ya muungano, kisha kwa hadhi inafuatia sheria ya Bunge, Kanuni na mwisho ni sheria ndogo.

Hii ina maana Profesa Assad ameitwa kwenye kamati ya bunge kutokana na hadhi (tabaka) yake, si kingine. Je, hilo lina maana iwapo baadhi yetu huku mitaani au kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii tukaandika au kusema Bunge ni dhaifu tunaweza kuachwa kwakuwa hatuna hadhi kama ya CAG kuitwa mbele ya Kamati? Je, CAG anaweza kuondolewa?

Ni kweli Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali anaweza kuondolewa kwa utaratibu iwapo ametimiza umri wa kuacha kazi kwa mujibu wa Ibara ya 144 kifungu cha kwanza (1).

Vilevile Ibara ya 144 kupitia kifunga cha pili (2) kinasema CAG anaweza kuondolewa iwapo hajatimiza vema majukumu yake, kushindwa kutekeleza kazi zake au kukumbwa na maradhi ambayo yanamnyima nafasi ya kutimiza wajibu wake. Sababu zote mbili zilizotajwa hapo juu bado hazimgusi Profesa Mussa Assad, kwakuwa ana afya njema na ametimiza wajibu wake vyema.

Aidha, Ibara ya 144(3)(a) na (b) zinasema Rais amepewa mamlaka ya kuunda Tume Maalumu inayoundwa na Majaji ya kuchunguza ambayo itamshauri Rais juu ya njia za kufanya, ikiwamo kumwondoa CAG kwa mujibu wa sheria. Spika amevunja Katiba?

CAG anayo kinga ya kutokuitikia wito wa kuhojiwa na mtu au taasisi yoyote nchini. Kinga husika ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ibara ya 143(6), inayosema; “Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3) na (4) ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo”.

Aidha, Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya Mwaka 2008 inatoa Kinga kwa CAG ya Kuhojiwa (kushtakiwa) kutokana na kazi yake. ‘Kuuza na kununua mgogoro’

Bunge letu vyovyote iwavyo bado limekuwa likilalamikiwa mambo mengi. Mbunge wake, Tundu Lissu alipigwa risasi, lakini hakukuwa na utaratibu wowote kuunda tume ya uchunguzi juu ya tukio hilo.

Kumekuwa na mijadala mingi inayopitishwa na Bunge kiasi kwamba inamlazimu Rais John Magufuli kuingilia kati. Mfano wa karibuni ni uamuzi wa kusitisha utekelezaji wa sheria ya kikokotoo ambayo ilipitishwa bungeni na kutungiwa kanuni na wizara husika.

Taifa letu lipo kwenye mtifuano mkubwa, matumizi ya mbegu za kutengenezwa (GMO) kiasi kwamba mkulima anatengenezewa mazingira ya kuwa tegemezi wa kila kitu. Ghala anategemea. Dawa anategemea. Soko anategemea. Na sasa mbegu anaporwa kutoka kwenye za asili hadi za maabara. Bunge letu lipo, halina kauli wala msimamo juu ya hilo kama mhimili ambao unatakiwa kuishauri na kusimamia serikali.

Bunge letu lipo wakati vivuko vya maeneo mbalimbali nchini vikiwa kwenye matatizo makubwa. Bunge letu ‘tukufu’ lipo na lilifahamu juu ya ubovu wa Kivuko cha Mv Nyerere. Yote hayo ni mambo ambayo yalitakiwa kuikumbusha serikali kutimiza wajibu wa kulinda usalama wa raia. Nini tafsiri ya hilo?

Kiongozi mmoja wa Bunge katika mazungumzo yetu yasiyo rasmi katikati ya wiki hii aliniambia kuwa kinachokosekana sasa ni nidhamu na kuheshimiana kwasababu kila mmoja ana sharubu, tunatoka taratibu katika utawala wa sheria unaozingatia mamlaka na wajibu wa kila mmoja.

“Spika angepungukiwa nini, kwanza watu waliishasahau, sasa akionyesha ambayo wameshindwa kushughulikia itakuwaje? Lakini je, CAG kama raia hana haki ya kutoa maoni? Je, maoni ni udhalilishaji?

Naamini kwa dhati kabisa kama viongozi walipaswa kuitana na kuzungumza kwa faragha nini tatizo na tunashughulikia vipi kwa sababu moja ya kazi ya Bunge ni kupitia na kuijadili taarifa ya mkaguzi.

Maana katika hili hakuna mshindi, ni kudhalilishana. Vilevile CAG anaweza kuitolea ufafanuzi na Spika akafedheheka zaidi. Ni sawa na mtu anayeamua ‘kununua mgogoro’ ambao haupo lakini anakazania kuwa ‘atakwenda kuuza mgogoro’ huo kwa wanunuzi asiowajua.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.