MATARAJIO YANAYOONGOZA KUUMIZA WATU KWENYE MAHUSIANO - 2

Mtanzania - - Rose -

HHABARI Anti, mimi ni msichana wa miaka 23, naishi Tanga, nina mpenzi wangu nimezaa naye mtoto mmoja tangu nijifungue ni mwaka wa tatu sasa hatujaonana.

Kwa kipindi chote hicho hatujawahi kuwasiliana wala hajawahi kuuliza maendeleo ya mtoto hivyo majukumu yote kuhusu mtoto natekeleza mwenyewe.

Kilichonifanya niombe ushauri kwa sasa ananipigia simu anaomba anioe, je, kwa mazingira hayo anaweza kuwa mume mwema kwangu. Jibu....

Pole kwa wakati mgumu ulionao, wanaume mara nyingi huwa wanawahi kusahau maumivu wanaowasababishia wanawake katika maisha hasa hili la kutelekeza watoto, hilo kwanza unapaswa kulifahamu.

Pili kwenye suala la kuomba mrudiane ili muweze kufunga ndoa unapaswa kupima mwenyewe kwa kile alichokutendea lakini zaidi angalia nafasi ya upendo aliyonayo katika nafsi yako.

Kama hutojali kuna vitu vya msingi unavyopaswa kuviangalia kabla ya kuchukua uamuzi kwanza je, ni nini kimemrudisha kwako, ni mapenzi ama maumivu ya alipotoka, pia uangalie zile tabia ambazo zimemfanya mpaka akamtelekeza mtoto ameshaziacha, ukipata majibu katika maswali hayo unaweza ukatoa uamuzi ambao hautakuathiri baadaye.

Mbali na hilo wanaume pia hujifunza kutokana na makosa, huenda ameshajitafakari ndiyo maana kaamua kujirudi kama amefanya hivyo unaweza kukubali akuoe, lakini lazima awe amebadilika kitabia.

Aidha, unapoamua kurudisha uhusiano unapaswa uhakikishe ameanza kumhudumia mtoto kikamilifu na pia usikubali kuishi naye kabla hajatimiza ahadi yake ya kufunga ndoa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.