MICHEZO

Mtanzania - - Habari Leo Ndani -

Sababu za Ozil kuwekwa benchi zatajwa

KOCHA wa timu ya Arsenal, Unai Emery, ameweka wazi sababu za kumuacha kiungo wake, Mesut Ozil, nje ya kikosi kilichokubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya West Ham, juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.

Kocha huyo amesema aliamua kumuacha benchi mchezaji huyo kwa sababu za kiufundi pia ni kutokana na Ozil kufanya mazoezi ya chini ya kiwango kwa kipindi cha wiki moja. Awali kulikuwa na taarifa kwamba, mchezaji huyo raia wa nchini Ujerumani bado alikuwa anasumbuliwa na tatizo la goti na ndio maana alikuwa benchi kwenye mchezo huo dhidi ya kikosi cha kocha Manuel Pellegrini.

Lakini Kocha Emery, hakuitaja sababu ya majeraha ya Ozil mara baada ya kuulizwa sababu za kumuacha kikosini mchezaji huyo.

“Niliamua kumpanga kila mchezaji ambaye alikuwa bora kwa ajili ya mchezo huo, tumekuwa tukishinda tukiwa na yeye na tukifungwa tukiwa na yeye, hivyo hakuna ukweli wowote juu ya kuwa kwenye mipango ya kumuuza mchezaji.

“Ukweli ni kwamba, wiki iliyopita Ozil alifanya mazoezi kwa kiwango cha chini, lakini napenda kuendelea kusema kwamba, siku zote tumekuwa tukishinda tukiwa naye na tukifungwa huku tukiwa naye,” alisema kocha huyo.

Ozil, mwenye umri wa miaka 30, amekuwa nje ya kikosi hicho cha Arsenal kwa michezo mitatu, huku akidaiwa kusumbuliwa na goti, lakini mchezaji huyo aliweka wazi kuwa afya yake imekaa sawa na amefanya mazoezi ya hali ya juu kwa wiki mzima kwa ajili ya kutaka kuitumikia klabu yake hiyo. Bao la pekee ambalo lilifungwa na Declan Rice katika dakika ya 48 liliweza kupeleka kilio kwa The Gunners, hivyo kuwa mara ya kwanza kwa Arsenal kufungwa na West Ham nje ya uwanja wa Emirates tangu walipofanya hivyo mwaka 2006.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.