Wanaharakati wakamatwa Loliondo

Mtanzania - - Habari Leo Ndani - Na ASHA BANI - DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelalamikia hatua ya polisi mkoani Arusha kuendelea kuwashikilia Clinton Kairungi, Supuk Maoi katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro.

Kukamatwa kwa wanaharakati hao wa migogoro ya ardhi katika eneo la Loliondo hadi sasa bado hakujawekwa wazi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Onesmo ole Ngurumwa, alisema hao ni watetezi wa haki za binadamu waliokamatwa Januari 7, mwaka huu kinyume na sheria za nchi kwa kuwaweka rumande katika Kituo cha Polisi Loliondo mpaka sasa.

Olengurumwa alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na hali inayoendelea ya mgogoro wa ardhi Loliondo siku hadi siku hali ambayo wanaharakati, wananchi wamekuwa wakikamatwa kila kukicha.

“Mtakumbuka kwamba hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu Loliondo imeendelea kuwa mbaya siku hadi siku.

“Ni mwaka juzi tulishuhudia ukiukwaji huo ikiwa ni pamoja na kuchomewa moto nyumba za wakazi na kunyang’anywa mifugo yao na hata wengine kuumizwa,’’ alisema Olengurumwa.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Jinai ya mwaka 1985, mtuhumiwa anapokamatwa anakuwa na haki mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuambiwa kosa analotuhumiwa nalo.

Nyingine ni kupewa dhamana, kuonana na ndugu, kupelekwa mahakamani kwa wakati na kuelezwa haki yake ya kupata msaada wa sheria.

“Hata hivyo, watetezi hawa baada ya kukamatwa na polisi hawakupatiwa haki yoyote kati ya haki zilizotajwa kwa mujibu wa sheria.

“Na katika kuthibitisha kwamba watuhumiwa walinyimwa haki zao za msingi, THRDC baada ya kupata taarifa ya kukamatwa kwa watetezi hawa ilimtuma Wakili Samsoni Rumembe na Msaidizi wa Sheria Charles Nangoya kwenda kuwapa msaada wa sheria lakini walizuiliwa,” alidai Ngurumwa.

Alisema vituo vya polisi vina vyumba vidogo vya kuhifadhi watuhumiwa kwa muda mfupi usiozidi saa 24.

“Polisi pia hawana chakula cha kulisha watuhumiwa, hawana madaktari wa kutibu watuhumiwa na taratibu nyingine za binadamu ambazo zipo katika magereza yetu.

“Hivyo kukaa na watuhumiwa zaidi ya wiki au zaidi ni kuvunja pia haki zao nyingine na wakati mwingine vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha vifo vya watuhumiwa au ulemavu na magonjwa,’’alisema

Alisema kwa hali inayoendelea sasa chini kwa chini kwa wananchi kuendelea kunyanyasika katika ardhi yao hapana budi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuingilia kati na Mkuu wa Jeshi la Polisi ( IGP) na kuwachukulia hatua wanaohusika moja kwa moja na ukandamizaji wa haki za binadamu.

Olengurumwa aliwataka watetezi na raia kwa mwaka huu uwe ni mwaka wa kudai haki mahakamani na si vinginevyo.

Alisema mtandao huo unakusudia kuwafungulia mashtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha na OCD kwa kuwashikilia watuhumiwa kwa muda mrefu kinyume na sheria.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’azi alisema anafuatilia tukio hilo na atakapopata maelezo ya kina atatoa ufafanuzi kwa umma.

MAZUNGUMZO: Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad. Kulia ni Mwenyekiti wa Ngome ya wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Yasin Mohamed.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.